Imewekwa: 24th Oct, 2020
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amezitaka Ofisi za umma, Taasisi na wananchi kwa ujumla kutumia maziwa yanayozalishwa nchini ili kuongeza uzalishaji wa maziwa na masoko kwa wafugaji na viwanda.
Mhe. Ulega amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa yaliyofanyika tarehe 25 Mei, 2020 mkoani Dodoma. Naibu Waziri Ulega amesema ni jambo la aibu kuona watanzania wakitumia maziwa ya unga na kuacha yale yanayotengenezwa na watanzania wenzao jambo ambalo amesema siyo la kizalendo.
Hivyo, Mhe. Ulega amesema Serikali itaanzisha kampeni ya kukagua Ofisi za Umma na binafsi ambazo zinatumia maziwa ya unga badala ya maziwa halisi yanayotengenezwa nchini.
“Leo ukipita katika ofisi za Serikali karibu zote zinatumia maziwa ya kopo yanayozalishwa nje ya nchi, huu sio uzalendo, lazima tuwe wazalendo kwa kuanza kupenda vya kwetu, ifike hatua tuone aibu kwa ofisi tena za serikali kunywa maziwa ya kopo”
Uzalishaji wa maziwa nchini umeongezeka kutoka lita bilioni 1.85 mwaka 2011/2012 na kufikia lita bilioni 3.01 mwaka 2019/2020 ambapo lita bilioni 2.1 sawa na asilimia 70 zinatokana na ng’ombe wa asili na lita milioni 900.3 sawa na asilimia 30 zinatokana na ng’ombe wa maziwa. Amesema sekta ya maziwa inachangia asilimia 1.2 ya pato la Taifa na kusisitiza unywaji wa maziwa kwa wingi utasaidia kutimiza ndoto ya Rais Dk John Magufuli kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
“Kama Taifa tukaamua kwa pamoja kunywa maziwa yetu yanayozalishwa hapa nchini tutakua siyo tu tunachangia pato la Taifa kwa kukuza uchumi bali tutaondoa umaskini kwani wafugaji na wauzaji wengi wa maziwa watafanya biashara kwa wingi," Amesema Ulega.
Naibu Waziri Ulega amesema serikali imekua ikiangaika kutafuta vyanzo vipya vya mapato lakini kama fursa ya biashara ya maziwa itatumika vizuri basi Tanzania itapiga hatua kubwa sana kiuchumi.
" Niwasihi watanzania wenzetu kuanza kutumia vya kwetu, unywaji wa maziwa kwa wingi utachangia sana ukuaji wa uchumi wetu, Shule ya Serikali na binafsi zinapaswa zianzishe utaratibu wa watoto wetu kunywa maziwa ili uwe kama Utamaduni wetu," Amesema Naibu Waziri Ulega.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amesema unywaji wa maziwa unachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha afya na kutoa rai kwa wananchi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla.
" Nitoe rai kwa watanzania kuwa na utaratibu wa unywaji maziwa, hii itasaidia kukuza uchumi wa Taifa letu lakini pia itachangia uimara wa afya zetu," Amesema DC Katambi.