Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
ULEGA AZINDUA PROGRAMU YA KOPA NG’OMBE LIPA MAZIWA
24 Jan, 2024
ULEGA AZINDUA PROGRAMU YA KOPA NG’OMBE LIPA MAZIWA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amezindua programu ya Kopa Ngo’mbe Lipa Maziwa yenye lengo la kuwainua kiuchumi vijana na kina mama hapa nchini.

Ulega amezindua programu hiyo katika hafla ya kukabidhi Ng’ombe 300 kwa Kampuni ya Kahama Fresh ambao watakopeshwa vijana na Wanawake waweze kujikwamua kiuchumi kupitia uzalishaji wa maziwa. Hafla hiyo imefanyika katika shamba la Mifugo la Kampuni ya Kahama Fresh lililopo wilayani Karagwe, mkoani Kagera Januari 23, 2024.

“Kwa dhati napenda kuipongeza kampuni ya Kahama Fresh kwa kutekeleza Programu ya Kopa Ng’ombe Lipa Maziwa inayolenga kukiwezesha kiwanda cha Maziwa cha Kahama Fresh kupata malighafi lakini pia kuwawezesha wafugaji wa Karagwe kuongeza uzalishaji wa maziwa na hivyo kujikwamua kiuchumi”, alisema

Pia, Waziri Ulega ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania – TADB kwa kutoa mkopo kwa kampuni ya Kahama Fresh ili iweze kununua mitamba bora 600 kwa jili ya kuongeza uzalishaji wa maziwa.

“Programu hii ya Kopa Ngómbe Lipa Maziwa imekuja kwa wakati muafaka na itaongeza kasi ya juhudi za Serikali kuleta mabadiliko ya sekta kupitia Wizara yangu. Hivyo, nawahimiza wafugaji kuwatunza ng’ombe watakaopewa ili kupata tija inayotarajiwa na kuhakikisha wanafuga kisasa”, alibainisha

Aidha, ameitaka TADB kuendelea kuwawezesha Watanzania wengi zaidi  ili waweze kufanya ufugaji wa Ng’ombe wa maziwa ili nchi iwe na uwezo wa kuzalisha maziwa mengi na kuwapelekea wahitaji katika nchi nyingine.

Waziri Ulega amekabidhi Ng’ombe 300 kwa awamu ya kwanza kati ya ngombe 600 ambao TADB imeikopesha kampuni ya Kahama Fresh ambao watawakopesha wafugaji ili waweze kuzalisha maziwa na kupeleka malighali kwenye kiwanda cha Kahama Fresh.

Programu ya Kopa Ng’ombe Lipa Maziwa inaendeshwa na kampuni ya Kahama Fresh kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo, Shirika la Heifer International na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.