Imewekwa: 24th Oct, 2020
Wafugaji wa maziwa mkoani Tanga wametakiwa kupanda malisho kwa wingi ili kuwasaidia kuzalisha maziwa mengi wakati wote.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa
Dkt. Sophia Mlote wakati wa kikao cha pamoja kati ya Bodi ya Maziwa Tanzania na
vyama vya msingi vya mkoa wa Tanga wakati wa kujadili mchakato wa kuwawezesha wafugaji
wa mkoa wa Tanga kununua mitamba 350 kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu
kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).
Bodi ya maziwa iliingia makubaliano rasmi na Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania, kwa lengo la kuviwezesha vyama vya ushirika vya
wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini kuwapatia mafunzo ya ufugaji bora na
mikopo nafuu kwa nia ya kuendeleza tasnia ya maziwa. Aidha, Mikopo kutoka TADB
itahusisha ununuzi wa ng’ombe bora wa maziwa, ujenzi wa mabanda, ununuzi wa
pembejeo kama vyakula na dawa za mifugo.
Dkt. Mlote ametoa wito kwa wafugaji kuhakikisha kuwa kila
mfugaji anaanzisha shamba la malisho kwa ajili ya mifugo aliyonayo. Aidha, Wafugaji waliitikia wito wa Bodi na Wizara
kwa kuomba maeneo yaliyofutiwa hati katika mkoa wa Tanga kama Amboni Estate,
Marungu, Kibaranga n.k kutengwa kwa ajili ya ngo'mbe wa maziwa ili wafugaji
wapate maeneo ya kuanzisha mashamba ya malisho ya mifugo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na vyama mbalimbali vya wafugaji
vya mkoa wa Tanga ambavyo vipo chini ya mwavuli wa Tanga Dairy Cooperative
Union (TDCU). Kwa mujibu wa taarifa ya
Mwenyekiti wa TDCU, katika mkoa wa Tanga kuna jumla ya vyama 26
na kati ya hivyo, vyama viwili vya Umoja wa Wafugaji Mwangoi (UWAMWA) na Chama
cha Ushirika wa Wafugaji Ng’ombe wa Maziwa Muheza (CHAWAMU) ndivyo
vilivyokamilisha mchakato wa kupata mkopo toka Benki ya Kilimo.
Dkt. Mlote, amesema kuwawezesha wafugaji mitaji ni moja ya
mikakati madhubuti inayofanywa na bodi ya maziwa kuwawezesha wadau kuwa karibu
na huduma za kibenki ili kuweza kujiinua kiuchumi.
Aidha, Msajili alisema kuwa wafugaji hawana budi kutumia
fursa hii ili kuongeza uzalishaji wa maziwa hapa nchini na kuviwezesha viwanda
vya kusindika maziwa kuzalisha kwa uwezo uliojengewa. Mpaka sasa uzalishaji wa
maziwa kwa nchi nzima ni lita bilioni 2.4 tu. Kwa uzalishaji huu, ulaji wa maziwa kwa mtu
kwa mwaka ni lita 47 kinyume na matakwa ya shirika la chakula duniani
linalomtaka kila mtu anywe maziwa lita 200 kwa mtu kwa mwaka.
Changamoto kubwa za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ni malisho duni, magonjwa na elimu ndogo ya
ufugaji na isiyozingatia kanuni bora wa ufugaji. Hali hii inasababisha kushuka
kwa kiwango cha uzalishaji wa maziwa hata kama mfugaji atakuwa na ng’ombe bora.
Bodi ya maziwa iliahidi kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji
wa maziwa kwa kushirikiana na taasisi nyingine mtambuka ili kuwasaidia wafugaji
kuzalisha maziwa bora na kwa wingi
zaidi.
Hatua hii imefikiwa ili kukamilisha mchakato wa zoezi
kubwa la kuwakabidhi wafugaji wa mkoa wa
Tanga mitamba bora yenye mimba kwa ng’ombe wa maziwa. Zoezi hili linatarajiwa kufanyika hivi
karibuni na Waziri mwenye dhama ya mifugo, Mhe. Luhaga Joelson Mpina.