WANAFUNZI ZAIDI YA 120,000 KUNUFAIKA NA HUDUMA YA MAZIWA SHULENI NCHINI

Wanafunzi wapatao 128,553 hapa nchini watanufaika na huduma ya maziwa shuleni kwa muda wa miaka miwili kwa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam ili kuboresha afya na kuongeza upatikanaji wa lishe bora shuleni.
Hayo yamesema Oktoka 8, 2025 wakati wa kikao chakutambulisha mradi wa kuimarisha soko la maziwa nchini, utakaowanufaisha zaidi ya wanafunzi 120,000 kwa kupeleka huduma ya maziwa shuleni sambamba na kuwanufaisha wafugaji 7,000 hapa nchini kupitia mradi huo.
Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) kwa asilimia 50 na Galaxy Food and Beverage Ltd asilimia 50, umezinduliwa Oktoba 8, 2025 katika Ukumbi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), jijini Dodoma, ukihudhuriwa na Bodi ya Maziwa Tanzania, Wizara ya Viwanda na Biashara, , wadau wa lishe, mashirika ya maendeleo, pamoja na taasisi mbalimbali za serikali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Nyango E. Mbogora, amesema kupitia mradi huo kwa kiasi kikubwa utasaidia kukuza viwanda vidogo vya uchakataji maziwa hapa nchini hali itakayopelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa maziwa hivyo itasidia upatikanaji wa lishe bora kwa wanafunzi wa shule za msingi kupitia maziwa yenye virutubisho na salama kwa afya.
Kwa mujibu wa maazimio ya kikao hicho, vigezo vya kuchagua shule zitakazonufaika na mradi huo vitahusisha shule zisizo na mpango wa maziwa, shule zenye changamoto za ufaulu na utoro, pamoja na maeneo yenye upatikanaji rahisi wa huduma za umeme kwa ajili ya uhifadhi wa bidhaa.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Bw. Joseph Semu, alisema Tanzania huzalisha lita bilioni 4.01 za maziwa kwa mwaka, huku lita bilioni 1 pekee zikichakatwa, hivyo mradi huo unatarajia kuongeza idadi ya shule na wanafunzi watakaonufaika na mradi huo apambo kwa sasa shule zipatazo 218 zenye wanafunzi 122,481 ndizo zinazotekeleza Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni .
Dkt. Winfrida Mayilla, Mkuu wa Programu wa GAIN, amesema matarajio ya mradi huo ni kuhakikisha wanafunzi wapatao 128,553 wanakunywa maziwa shuleni, kuchakata lita 29,000 za maziwa kwa siku na kuongeza kipato cha Watanzania kupitia thamani ya bidhaa za maziwa.
Aidha, Meneja wa Viwanda wa Galaxy Food and Beverages Ltd, Bw. Fidelis Madzorera, ameeleza kuwa mradi huo utazingatia usalama wa mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kupitia matumizi ya nishati ya jua katika vituo 22 vya ubaridi vitakavyoanzishwa.