Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
TDB YASISITIZA USALAMA WA MAZIWA KWA WANAFUNZI SHULENI
24 Oct, 2025
TDB YASISITIZA USALAMA WA MAZIWA KWA WANAFUNZI SHULENI

Mtekinolojia wa Chakula kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania, Bw. Deogratius Buzuka, ametoa wito kwa wadau wa sekta ya maziwa nchini kuhakikisha maziwa yanayotumiwa katika shule ni salama na yenye ubora unaokubalika, ili kulinda afya za watoto na kuendeleza Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni.

Akizungumza katika Kongamano la Wadau wa Maziwa Mkoa wa Geita hivi karibuni, Bw. Buzuka alisema usalama wa maziwa ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa mpango wa unywaji maziwa shuleni unaoratibiwa na Bodi ya Maziwa Tanzania. Alibainisha kuwa, pamoja na juhudi za kuongeza unywaji wa maziwa, ni muhimu kuhakikisha maziwa hayo yanapitia hatua zote za ukaguzi, uchakataji, na uhifadhi salama.

“Tunahitaji kuhakikisha kuwa kila tone la maziwa linalofika kwa mtoto shuleni ni salama, limehifadhiwa vizuri na limekidhi viwango vya ubora,” alisema Buzuka.

Aliongeza kuwa maziwa yasiyotunzwa vizuri yanaweza kusababisha magonjwa ya tumbo na kupunguza uaminifu wa wazazi na jamii katika Mpango wa Maziwa Shuleni. Alisisitiza umuhimu wa elimu kwa wazalishaji na wasindikaji juu ya usafi, uchakataji sahihi na matumizi ya vifaa vinavyokidhi viwango vya ubora.

Bw. Buzuka pia aliwataka wadau wote – wakiwemo wazalishaji, wasindikaji, shule na taasisi za serikali kushirikiana kuhakikisha kuwa mnyororo mzima wa maziwa kutoka shambani hadi kwa mlaji unazingatia kanuni za usalama wa chakula.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa Tasnia ya Maziwa, wakiwemo Wafugaji, Wasindikaji, Viongozi wa Serikali, na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayojihusisha na Maendeleo ya Tasnia ya Maziwa nchini.