IRINGA YAANZA MAANDALIZI YA WIKI YA MAZIWA 2026
Mkoa wa Iringa umeanza rasmi maandalizi ya Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa 2026 baada ya kufanyika kikao cha kwanza cha wadau wa sekta ya maziwa kilichofanyika Machi 4, 2026, kikilenga kupanga mikakati ya kufanikisha maadhimisho hayo yanayotarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa tasnia ya maziwa nchini.
Kikao hicho kilihusisha wadau kutoka taasisi za Serikali, sekta binafsi, na wadau wa Sekta ya Maziwa wa mkoa wa Iringa, ambapo kilijadili maandalizi ya awali ya shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika kipindi cha wiki hiyo pamoja na namna ya kuhamasisha uzalishaji, uchakataji na matumizi ya maziwa nchini.
Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Bi. Dorinidei Mng'ong'o ambaye ni Kaimu Meneja Ufundi Maziwa alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kufanikisha maadhimisho ya Wiki ya Maziwa, akieleza kuwa tukio hilo ni jukwaa muhimu la kuhamasisha matumizi ya maziwa, kukuza biashara na kuonesha fursa zilizopo katika tasnia ya maziwa.
Katika kikao hicho, Meneja Masoko wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Bw. Joseph Semu, aliwasilisha andiko la maandalizi ya Wiki ya Maziwa 2026 lililoeleza malengo ya maadhimisho hayo, shughuli mbalimbali zitakazofanyika pamoja na ushiriki wa wadau katika kuendeleza tasnia ya maziwa nchini.
Kikao hicho kiliazimia kuunda kamati ndogo za maandalizi ya shughuli mbalimbali za Wiki ya Maziwa, kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya maziwa, kuanza mapema kampeni za uhamasishaji wa matumizi ya maziwa kwa umma, pamoja na kuhakikisha maandalizi yote muhimu yanakamilika kwa wakati ili kufanikisha maadhimisho ya Wiki ya Maziwa 2026 kwa ufanisi.
