DKT. MADELE AHAMASISHA WANANCHI KUSHIRIKI WIKI YA MAZIWA 2026
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, , ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Maziwa 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Mwembetogwa Mkoani Iringa.
Dkt. Madele ametoa wito huo Mei 29, 2026 mara baada ya kutembelea na kukagua mabanda ya maonesho ya wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo na maziwa wanaoshiriki maadhimisho hayo, ambapo amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuhamasisha unywaji wa maziwa na kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.
Amesema miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia Tasnia ya Maziwa inalenga kuleta mageuzi makubwa katika Tasnia hiyo kwa kuwasaidia wafugaji kupata ng’ombe bora wa maziwa pamoja na kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa mbegu na mifugo bora.
“Miradi hii inalenga kuongeza tija kwa wafugaji wetu na kuhakikisha Tasnia ya Maziwa inakuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Madele.
Aidha, amebainisha kuwa sekta ya maziwa ni miongoni mwa Tasnia zenye fursa kubwa za kiuchumi kwani inanufaisha wafugaji, wasindikaji, wafanyabiashara pamoja na makampuni mbalimbali yanayojihusisha na shughuli za uzalishaji na usindikaji wa maziwa nchini.
Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa 2026 yanaendelea Mkoani Iringa huku yakitoa nafasi kwa wananchi kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa, kupata elimu ya ufugaji bora na kujionea fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa Tasnia ya Maziwa.
