MAADHIMISHO YA WIKI YA MAZIWA KUNOGESHWA NA MRADI WA MAGEUZI YA TASNIA YA MAZIWA NA MABADILIKO YA TABIANCHI
Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa yanayotarajiwa kufanyika Mkoani Iringa kuanzia Mei 25 hadi Juni 01, 2026 yanataria kuvutia wadau mbalimbali wa Tasnia ya Maziwa huku Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (Climate Smart) ukiwa miongoni mwa miradi inayotoa matumaini mapya kwa wafugaji na wazalishaji wa maziwa nchini.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari Mei 25, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James alisema maadhimisho hayo yanalenga kuonesha mafanikio na fursa zilizopo katika Tasnia ya Maziwa sambamba na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira kupitia miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi.
Mhe. Kheri James alieleza kuwa mradi huo unasaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa kutumia mbinu zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ufugaji bora, uhifadhi wa malisho, matumizi sahihi ya maji pamoja na kuongeza ufanisi katika uzalishaji na uhifadhi wa maziwa.
Aidha, alisema kuwa kupitia maadhimisho hayo wananchi na wadau watapata nafasi ya kujifunza teknolojia mpya, kutembelea mabanda ya maonesho pamoja na kupata elimu kuhusu mchango wa Tasnia ya Maziwa katika kuboresha lishe, kuongeza kipato na kukuza uchumi wa taifa.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, Iringa imejipanga kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanyika kwa mafanikio makubwa huku akiwakaribisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Mwembetogwa vilivyopo Manispaa ya Iringa kushiriki shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika kipindi chote cha Wiki ya Maziwa.
Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa mwaka 2026 yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha wadau wa Tasnia ya Maziwa na kuendeleza ajenda ya uzalishaji endelevu unaozingatia mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
