Promosheni
Huduma za Uhamasishaji
1. Kufanya shughuli za kitaifa za uhamasishaji wa unywaji maziwa
Bodi ya Maziwa Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na wadau mbalimbali wa maziwa kila mwaka imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Maziwa Kitaifa ambayo huwa inafanyika kuanzia mwishoni mwa mwezi Mei hadi mwanzoni mwa mwezi Juni.Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa yalianza yakiwa na dhana ya kuhamasisha unywaji wa Maziwa na kuboresha soko la maziwa, dhana hiyo imekuwa ikibadilika na maadhimisho hayo kwa sasa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita yanalenga kuboresha wadau wote walioko kwenye mnyororo wa thamani (Value Chain) kuanzia mfugaji mpaka mlaji.
Malengo ya Wiki ya Maziwa
Malengo ya Wiki ya Maziwa ni kama yafuatavyo:
a) Kuelimisha wananchi na umma matumizi ya maziwa kama chakula bora kwa watu wa rika zote na faida za maziwa katika kujenga afya ya binadamu.
b) Kuwashawishi watunga sera umuhimu wa tasnia ya maziwa katika kukuza uchumi wa nchi na kuondoa umasikini.
c) Kuwaelimisha wadau kuongeza ubora wa bidhaa za maziwa zinazotengenezwa nchini
d) Kuwaelimisha wadau umuhimu wa kujiunga na vyama vya Ushirika
e) Kuwa na jukwaa linalowakutanisha wadau wa tasnia ya maziwa ambao litawawezesha kubadilishana ujuzi na uzoefu na kujifunza baina ya wadau wa maziwa. Kwahiyo, katika Wiki ya Maziwa shughuli zingine muhimu za wadau zinafanyika sambamba na maonesho nazo ni Mkutano wa Baraza la Wadau wa Maziwa ambalo lipo Kisheria, Jukwaa la Wadau wa Maendeleo la Tasnia ya Maziwa
f) kuwahamasisha wadau kunywa maziwa yaliyosindikwa kwa ajili ya usalama na ubora wake
2. Kuhamasisha mpango wa unywaji maziwa mashuleni
Bodi ya Maziwa Tanzania inahamasisha na kuratibu mpango wa Unywaji maziwa shuleni. Mpango ulianzishwa mwezi Juni 2001 wakati wa wiki ya uhamasishaji wa unywaji maziwa iliyofanyika kitaifa huko Arusha. Mpango ulianza mwishoni mwa mwaka wa 2001 na mapema mwaka 2002 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro (sehemu ya kaskazini mwa Tanzania) kama mradi wa majaribio. Mpango huu ulianzishwa kwa juhudi za serikali, wadau na wazazi. Juhudi za wadau mbalimbali zimeweza kuanzisha mipango midogo midogo ya maziwa shuleni kwa wazazi kushirikiana na wasindikaji na ufadhili wa asasi mbalimbali kama Halmashauri za Manispaa, mashirika ya kitaifa na kimataifa.
Kwa sasa Programu ya Unywaji wa Maziwa Shuleni ambayo inatekelezwa kwenye shule 45 na hunufaisha jumla ya wanafunzi 31,974 kwenye wilaya za Arusha, Hai, Moshi, Njombe, Rungwe na Tanga. Hii inaonyesha kuwa kwa ushirikiano wa walimu, wazazi, viwanda vya kusindika maziwa, viongozi wa serikali na wa kisiasa na wafadhili mbali mbali, mpango wa maziwa shuleni hata hapa nchini unaweza kuwa wa kitaifa.
Mpango huu una malengo yafuatayo;
a) Kuongeza mahitaji ya maziwa nchini
b) Kupanua soko la maziwa
c) Kupanua utamaduni wa kunywa maziwa kwenye jamii na hivyo kuongeza wastani wa kunywa maziwa kwa kila mtu nchini.
3. Kuhamasisha Uwekezaji kwenye Tasnia ya Maziwa
Bodi ya Maziwa imekuwa ikihamasisha wadau kuwekeza kwenye sekta ya maziwa katika maeneo ya uzalishaji, usindikaji na masoko.Tasnia ya maziwa inachangia takribani theluthi moja ya 4.6% ya mapato yatokanayo na mifugo kwenye mapato ghafi ya Taifa. Hivyo basi, Tasnia ya maziwa inafursa kubwa katika kuchangia kwenye usalama wa chakula, ajira na kipato cha mwananchi.
4. Kuwa Kipaumbele
Bodi itaendelea kuwa kipaumbele katika masuala yanayohusu Tasnia ya Maziwa katika sera, uzalishaji, usindikaji, teknolojia, masoko na nyinginezo