Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
Taratibu za uingizaji wa maziwa na bidhaa za maziwa nchini

Usajili wa Wadau

Tasnia ya Maziwa hapa nchini inasimamiwa na Sheria ya Maziwa sura 262 kifungu cha 17 (1-2) ya Mwaka 2004. Sheria hii ilitungwa kutokana na kuwepo kwa ombwe katika usimamizi wa tasnia ya maziwa baada ya kuvunjwa kwa mamlaka ya kusimamia na kuendeleza mifugo na mazao yake (Livestock Development Authority - LIDA) mwanzoni mwa miaka ya 1980. Vile vile kumekuwepo na hitajio la maziwa bora na salama katika soko la ndani na nje ya nchi.

Bodi ya Maziwa Tanzania iliundwa kwa lengo la kuweka misingi thabiti ya kuendeleza uzalishaji, usindikaji, biashara ya maziwa na mazao yake inayozingatia ubora na viwango ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. Aidha, katika kutekeleza majukumu hayo Bodi haina budi kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo Bodi imeandaa kanuni na miongozo ya uzalishaji,usindikaji, ukusanyaji, masoko na usajili wa wadau wa tasnia ya maziwa ili kuelekeza wadau katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu ya sheria. Ili kutekeleza usajili ni dhahiri kuwa ukaguzi ndio ufunguo wa utambuzi na usajili wa wadau wa Tasnia ya Maziwa.

Lengo la Usajili

Kuwezesha wadau kushiriki kikamilifu katika kuendeleza tasnia ya maziwa kuanzia kwenye uzalishaji, usindikaji, biashara ya mifugo, maziwa na mazao yake. Vile vile inawezesha wadau kupatiwa huduma mbalimbali zikiwemo taarifa muhimu za tasnia na kuunda mtandao baina yao.

Wadau na maeneo yatakayosajiliwa

Watakaosajiliwa na kutambuliwa ni watu binafsi, taasisi, vyama vya kijamii kampuni na maeneo yanayotumika katika uzalishaji wa maziwa na bidhaa zake, katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani wa zao la maziwa kibiashara. Wadau na maeneo hayo ni pamoja na:-

  1. Wazalishaji wa maziwa,
  2. Wasindikaji wa maziwa
  3. Wakusanyaji wa maziwa
  4. Wasafirishaji wa maziwa
  5. Wachuuzi
  6. Waagizaji na wanunuzi wa maziwa ndani au nje ya nchi
  7. Wauzaji wa pembejeo
  8. Wauzaji wa rejareja wa maziwa

Maombi ya usajili wa wadau wa maziwa

Mtu yeyote kabla ya kufanya biashara ya maziwa yoyote lazima apate usajili kutoka Bodi ya Maziwa. Utaratibu wa usajili unahitaji mwombaji kujaza na kuwasilisha fomu ya maombi ya usajili kutoka kwa Msajili. Fomu ya Maombi ya Usajili inapatikana katika ofisi za Bodi za Maziwa na inaweza kupakuliwa kwenye tovuti.

Mshiriki yeyote wa maziwa, kabla ya kusajiliwa, atakubaliana na masharti yaliyowekwa katika kanuni kama ifuatavyo;

Sr. no.

Wadau

Masharti kabla ya Usajili

1.

Mzalishaji wa maziwa

(1) Uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita 10 kwa siku

(2) Awe na sehemu safi ya kuzalisha maziwa

(3) Awe na vifaa safi vya kuhifadhia maziwa

(4) Aweze kufuata taratibu na kanuni za uzalishaji bora wa maziwa

(5) Aweze kufuata kanuni za usafi na uhifadhi wa maziwa

2.

Mkusanyaji wa maziwa

(1) Awe na vifaa vya kuhifadhi maziwa

(2) Afuate kanuni za usafi na uhifadhi wa maziwa

(3) Awe na matenki ya kupoozea maziwa

(4) Awe na vifaa vya kuangalia ubora wa maziwa

(5) Awe na jengo maalumu na salama kwa ajili ya kukusanyia maziwa

3

Mchuuzi

(1) Awe na vifaa vya kuhifadhia maziwa

(2) Afuate taratibu na kanuni za usalama wa maziwa

(3) Awe na vifaa vya kupima ubora wa maziwa

4.

Msafirishaji wa maziwa

(1) Awe na chombo kilichothibitishwa kwa ajili ya kusafirisha maziwa

5.

Msindikaji wa Maziwa

(1) Awe na leseni iliyothibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa

6.

Muingizaji/mtoaji wa maziwa ndani na nje ya nchi/ msambazaji

(1) Awe na leseni iliyothibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa

7.

Muuzaji wa pembejeo

(1) Leseni ya biashara


Kwa ufafanuzi zaidi wasiliana na Bodi ya Maziwa Tanzania.