WADAU WAPATAO 138 WAPATA MAFUNZO YA USINDIKAJI BORA WA MAZIWA

Wadau zaidi ya 138 wapatiwa mafunzo ya usindikaji bora wa maziwa kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya 28 ya Wiki ya Maziwa yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Morogoro kuanzia Mei 27 hadi Juni Mosi 2025 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.
Mafunzo hayo yaliyowashirikisha Washiriki mbalimbali kutoka katika Halmashauri na mikoa ya Tanzania Bara yalikuwa na lengo la kuwajengea uwezo wa kuweza kuyatambua maziwa yasiyofaa kwa ajili ya kulinda afya ya walaji sambamba na kufundishwa namna ya kusindika maziwa
Akitoa Mafunzo hayo Mtekinolojia wa Chakula kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania Bw. Rajilan Hilal ameeleza kuwa wananchi wengi wanatumia maziwa yasiyofaa kwa afya zao hivyo mafunzo hayo yamelenga kuwafundisha Maafisa Mifugo, Maafisa Lishe na wadau mbalimbali walitoka katika Halmashauri zote nchini ili watakapofika kwenye maeneo yao ya kazi kueneza elimu hiyo kwa wananchi ili waweze kutumia maziwa safi na salama kwa afya zao.
Ameendelea kusema kuwa Maziwa salama ni yale yaliyohakikiwa ubora na yaliyozingatia mifumo ya kisasa ya uzalishaji ambayo yatakuwa salama kwa mtumiaji wa mwisho.
‘Tunapotoa mafunzo haya sisi kama Bodi ya Maziwa tunategemea kuwa wakitoka hapa wataenda kueneza elimu hii kwa wananchi wanaowasimamia huko kwenye maeneo yao hii itasaidia kupunguza wimbi la matumizi ya maziwa yasiyofaa’ Amesema Bw. Rajilan
Wakishukuru kwa nyakati tofauti, Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Songea Bi. Alice ameishukuru Bodi ya Maziwa Tanzania kwa kuweza kuendesha mafunzo hayo kwani wamepata uelewa mkubwa wa namna ya usindikaji bora wa maziwa kwani hawakuwa wanajua kusindika maziwa kwa kutumia njia za kitaalamu hivyo elimu hii itamsaidia katika majukumu yake ya uhamasishaji wa lishe bora kwa wananchi wa Songea.
Bodi ya Maziwa Tanzania imekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wananchi na wadau wa maziwa ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa.