Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
VITUO 23 VYA KUKUSANYIA MAZIWA VYAZINDULIWA
04 Mar, 2026
VITUO 23 VYA KUKUSANYIA MAZIWA VYAZINDULIWA

Serikali imezindua rasmi vituo 23 vya kukusanyia maziwa katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayotajwa kuwa chachu mpya ya kuimarisha tasnia ya maziwa na kuongeza kipato kwa wafugaji.

Uzinduzi huo uliofanywa Mchi 02, 2026 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Bashiru Ally Kakurwa mkoani Kagera kwa niaba ya vituo vingine nchini umeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa maziwa na kuimarisha mnyororo wa thamani kuanzia ngazi ya mfugaji hadi viwandani. Vituo hivyo vinatarajiwa kupunguza upotevu wa maziwa, kurahisisha ukusanyaji na kuhakikisha maziwa yanahifadhiwa katika mazingira salama kabla ya kusafirishwa kwa ajili ya uchakataji.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Bashiru alisema vituo hivyo vitarahisisha ukusanyaji wa maziwa, kupunguza upotevu wa mazao na kuboresha ubora wa maziwa kabla ya kufikishwa viwandani kwa ajili ya uchakataji. Alieleza kuwa miundombinu hiyo ni kichocheo muhimu cha kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa kuanzia kwa mfugaji hadi sokoni.

“Serikali imejipanga kuhakikisha wafugaji wanapata soko la uhakika na bei yenye tija. Vituo hivi vitasaidia kuongeza uzalishaji, kipato na ajira kwa wananchi wa Kagera,” alisema Waziri huyo.

Mtendaji Mkuu wa Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Frank Nyabundege alisema benki hiyo itaendelea kuwawezesha wafugaji na vikundi vyao kupata mikopo nafuu kwa ajili ya kuboresha mifugo, miundombinu ya uzalishaji na vifaa vya kuhifadhia maziwa, ili kuongeza tija na ubora wa mazao yao.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Heifer Bw. Mark Txsoso amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuwawezesha wafugaji kupitia mafunzo ya ufugaji bora, lishe ya mifugo na usimamizi wa biashara, ili kuhakikisha vituo hivyo vinakuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa jamii.

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Prof. George Msalya alisema Bodi itaendelea kusimamia ubora na usalama wa maziwa yanayokusanywa katika vituo hivyo, sambamba na kuhamasisha matumizi ya maziwa nchini ili kuongeza soko na kuimarisha tasnia ya maziwa kwa manufaa ya wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Uzinduzi wa vituo vya Nshamba na Maruku umeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali za kuimarisha sekta ya mifugo na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wafugaji wa ngazi ya chini, hususani katika maeneo ya vijijini.

Kwa upande wao, wawakilishi wa wafugaji wamepongeza hatua hiyo wakisema vituo hivyo vitawapunguzia gharama za usafirishaji na changamoto ya kuharibika kwa maziwa kutokana na uhifadhi usio bora. Wameahidi kuongeza uzalishaji ili kunufaika kikamilifu na fursa hiyo.

Wadau wa sekta ya maziwa wameeleza kuwa uzinduzi wa vituo 23 vya kukusanyia maziwa ni hatua muhimu katika safari ya kuifanya Tanzania kuwa na tasnia ya maziwa yenye ushindani, inayozalisha kwa wingi na kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.