Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
FRAUKE JONGBLUTH AIPONGEZA ASAS, AONA FURSA ZA KUINUA TASNIA YA MAZIWA
20 Feb, 2026
FRAUKE JONGBLUTH AIPONGEZA ASAS, AONA FURSA ZA KUINUA TASNIA YA MAZIWA

Meneja Uendeshaji kutoka Benki ya Dunia, Bi. Frauke Jongbluth, ameipongeza Kampuni ya ASAS kwa uwekezaji wake katika uchakataji wa maziwa na kuona fursa kubwa zinazoweza kuinua tasnia ya maziwa nchini, baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo mkoani Iringa nakufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bw. Fuad Jaffer tarehe 19 Februari, 2026.

Katika mazungumzo yake na Mkurugenzi wa Kiwanda hicho pamoja na ujumbe alioambata nao, ameweza kupata taarifa mbalimbali iliyokuwa na lengo la Bi. Jongbluth alitembelea maeneo mbalimbali  za uchakataji, ufungashaji na udhibiti wa ubora wa bidhaa za maziwa zinazozalishwa na kiwanda hicho, huku akipata maelezo kuhusu uwezo wa uzalishaji, soko na mchango wa kiwanda katika ajira na uchumi wa ndani.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Bi. Jongbluth alisema uwekezaji unaofanywa na ASAS unaonesha namna sekta binafsi inavyoweza kuchochea maendeleo kupitia kuongeza thamani ya mazao ya ndani na kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa kuanzia kwa mfugaji hadi kwa mlaji.

“Ni jambo la kutia moyo kuona uwekezaji wa aina hii unaoongeza thamani ya maziwa, unaoongeza ajira na unaochangia katika kuboresha ubora wa bidhaa. Haya ni maeneo yenye fursa kubwa ya kuendelea kuinua tasnia ya maziwa,” alisema Bi. Jongbluth.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kiwanda cha ASAS, Bw. Fuad, alisema kiwanda hicho kimejikita katika kuongeza uwezo wa uzalishaji kwa kuboresha teknolojia, kuimarisha ubora wa bidhaa na kupanua masoko ili kukidhi mahitaji ya ndani na nje ya nchi.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya ukuaji wa tasnia ya maziwa nchini. Lengo letu ni kuongeza uzalishaji na kuhakikisha bidhaa zetu zinakidhi viwango, huku tukishirikiana na wazalishaji wa maziwa na wadau wengine katika mnyororo mzima,” alisema Bw. Fuad.

Naye Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania alisema Bodi inaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa tasnia ya maziwa, hususani viwanda vya kuchakata maziwa kama ASAS, ili kuimarisha uzalishaji, ubora na usalama wa maziwa yanayozalishwa nchini. 

Aliongeza kuwa ushirikiano huo unalenga kuongeza soko la uhakika kwa wafugaji, kuimarisha viwango vya bidhaa na kuchochea ukuaji wa tasnia kwa maendeleo ya Taifa.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya wadau wa maendeleo na sekta binafsi, kwa lengo la kuendelea kuchochea uwekezaji wa viwanda na kuongeza mchango wa tasnia ya maziwa katika uchumi wa nchi.