Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
WIKI YA MAZIWA MOROGORO YAIBUA WADAU WAPYA 22 KWENYE TASNIA YA MAZIWA NCHINI
25 Jun, 2025
WIKI YA MAZIWA MOROGORO YAIBUA WADAU WAPYA 22 KWENYE TASNIA YA MAZIWA NCHINI

Itakumbukwa kuwa kila mwaka Bodi ya Maziwa kwa kushirikiana na wadau wake hapa nchini huadhimisha Wiki ya Maziwa kwa kuhamasisha matumizi ya maziwa hasa yaliyosindikwa na bidhaa zake ambapo kwa mwaka 2025 Maadhimisho hayo yamefanyika mkoani Morogoro na kuwezesha kupata wadau wapya wapatao 22 kwenye mnyororo wa thamani wa maziwa.

Wadau hao ambao ni Wasindikaji, Wasafirishaji, Wafugaji na Wafanyabiahara wa maziwa waliweza kusajiliwa na Bodi ya Maziwa Tanzania wakati wa Maadhimisho ya 28 ya Wiki ya Maziwa yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege,  Manisapa ya Morogoro kuanzia Mei 27 hadi Juni Mosi 2025.

Akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Afisa Mteknolojia wa Chakula Bw. Kennedy Daniel amesema kuwa kuwapata wadau hao wapya ni kielelezo kuwa Tasnia ya Maziwa nchini inaendelea kukua siku kwa siku ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita hivyo amewahimiza wadau ambao bado hawajajisajili wafanye hivyo kwa mstakabali mzima wa Tasnia ya Maziwa.

‘Wapo watu wengi wanaofanya biashara ya maziwa bila kufuata sheria,  kanuni na taratibu, mojawapo ikiwa ni sharti la kusajiliwa na Bodi ya Maziwa nchini iliyopewa jukumu ya kusimamia Tasnia ya Maziwa kisheria hivyo niwasihi wale wote wanaofanya biashara ya maziwa nchini kuhakikisha wanasajiliwa’ Amesisitiza Bw. Kennedy

Vilevile amebainisha faida za Kusajiliwa na Bodi ya Maziwa kuwa itamuwezesha mdau kutambuliwa na Bodi hiyo yenye jukumu la kusimamia Tasnia ya Maziwa, ambapo  itakuwa na jukumu la kumsaidia kwa karibu pale anapokutana na changamoto kwenye mnyororo mzima wa thamani wa maziwa ikiwa ni pamoja kumtafutia masoko ya maziwa pale anapokwama pamoja na kumfungulia fursa mbalimbali zilizopo kwenye Tasnia ya Maziwa.