BODI YA MAZIWA YATOA TAHADHARI UNYWAJI MAZIWA YANAYOUZWA HOLELA MTAANI
Bodi ya Maziwa Tanzania imetoa tahadhari ya Unywaji maziwa yanayouzwa kiholela mtaani kwani husababisha madhara makubwa kwa walaji kwakuwa hutoka moja kwa moja kwa mfugaji na kufungashwa katika chupa za plastiki ambazo sio vifungashio rasmi vya maziwa.
Hayo yamesemwa na Msajili wa Bodi hiyo Profesa George Msalya wakati akiwasilisha mada katika warsha ya waandishi wa habari iliyofanyika Mei 21, 2024 katika ukumbi wa TVLA jijini Dar Es Salaam ikiwa na lengo la kuwajengea uwelewa Waandishi hao kuelekea Maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maziwa Kitaifa yanayotarajiwa kufayika mkoani Mwanza Mei 28, 2024 mpaka Juni 01, 2024.
K wa mujibu wa Prof Msalya suluhisho pekee la kunywa maziwa salama ni muhimu kutumia maziwa yaliyotoka viwandani kwani ni salama kwakuwa taratibu zote za kiafya hufuatwa kwenye maandalizi.
Akizungumzia usalama wa maziwa ya viwandani, Ofisaa Maendeleo ya Biashara Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Edmund Mariki amesema maziwa yasipopita kiwandani na mtu akayatumia athari inaweza kujitokeza kama ng’ombe ametumia dawa na ana maradhi.
‘Maziwa yanapopita viwandani ni salama zaidi kwa sababu wanabaini ubora kabla ya kupeleka kwa mlaji, yakiwa na shida hayawezi kuhifadhiwa kupelekwa kwa mlaji,’ amesema
Maziwa huchemshwa kitaalamu kwa dakika 30 kwa nyuzi joto 65 kutokana na vimelea vilivyopo kwenye maziwa hupoteza uhai kwa joto hilo hivyo kwa mtu aliye nyumbani anayehitaji kuchemsha maziwa kuua vimelea hupaswa kutenga chombo maalumu chenye maji na kutumbukiza chombo kingine chenye maziwa , kuchemsha kwa joto hilo taratibu na baadaye kuyapooza na kuyahifadhi kwenye jokofu.
Naye kaimu Meneja Ufundi Maziwa TDB, Bi Dorinidei Mng’ong’o amesema chanzo cha maziwa kuharibika ni kutozingatiwa usafi wa ng’ombe anayekamuliwa, uchafu wa mkamuaji, kuongezwa maji kwenye maziwa, vyombo vya kuhifadhi maziwa na kusafirishia maziwa.