Imewekwa: 29th Nov, 2022
Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Maziwa Tanzania wakishirikiana na Chama cha Wafugaji wa Mkoa wa Tanga hivi karibuni wamewatembelea na kuona maendeleo ya wafugaji wa mkoa huo walipofanya ziara ya siku moja mkoani humo lengo likiwa kupata changamoto zinazowakabili wafugaji hao.
Katika ziara hiyo wameweza kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji hao ikiwa ni pamoja na uhaba wa malisho kwa wafugaji hao hali inayopelekea upatikanaji mdogo wa maziwa kwa ng’ombe wanaokamuliwa kwani ili ng’ombe aweze kutoa maziwa mengi ni lazima kuwe na uhakika wa malisho ya kutosha.
Kwa upande wa wafugaji kupitia kwa mwenyekiti wa chama Ushirika cha wafugaji cha UWABU kilichopo Kange Bwana Vincent Charles wameiomba serikali kuwawezesha kuwapatia wataalamu wa mifugo wa kutosha kwenye maeneo yao ili waweze kuwatumia pindi wanapokumbana na changamoto za hapa na pale hasa kipindi cha magonjwa.
Pia wameiomba serikali kupitia kwa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo kuwawezesha kuwapatia mbegu bora za kupandishia ng’ombe kwa mara moja kwani kwa kipindi kirefu wamekuwa wakisumbuka kuwapandisha ng’ombe zaidi ya mara 4 hivyo inawasababishia hasara kwao.
Bodi yaUshauri ya Bodi ya Maziwa Tanzania katika ziara hiyo imeahidi kushirikiana na wafugaji wa mkoa wa Tanga kuhakikisha madai ya wafugaji yanapatiwa ufumbuzi mapema kwa mtakabali wa maendeleo ya mifugo hapa nchini kwani Mkoa wa Tanga ni moja ya mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa Maziwa hapa nchini.