Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
Dkt. Mshote: AWATAKA WADAU MBALIMBALI KUWEZESHA WATOTO KUPATA MAZIWA SHULENI
11 Dec, 2023
Dkt. Mshote: AWATAKA WADAU MBALIMBALI KUWEZESHA WATOTO KUPATA MAZIWA SHULENI

Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Elizabeth Mshote amewataka wadau mbalimbali hapa nchini wakiwemo Maafisa Lishe, Wakuu wa Shule kuweka mikakati itakayowezesha watoto kupata maziwa wawapo shuleni 

Ametoa kauli hiyo Desemba 7, 2023 kwenye Uzinduzi wa Mpango wa Uhamasishaji Unywaji maziwa shuleni ulioenda sambamba na utambulisho wa bidhaa mpya sokoni wa mtindi laini ulioongezwa virutubisho ili kupambana na tatizo la Udumavu na Utapia mlo kwa watoto ambapo alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam. 

Dkt. Mshote ameeleza kuwa Unywaji wa Maziwa kwa watoto unawezesha watoto kuwa na afya bora na hivyo kuwezesha kuwa na ufaulu mzuri katika masomo yao na hivyo kuwa na Taifa lenye watu bora kiafya na kifikra. 

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Dkt. George Msalya amesema kuwa katika kupambana na hali ya Udumavu nchini Serikali kupitia Taasisi ya Bodi ya  Maziwa nchini imeweka mpango jumuishi wa lishe ambapo imepanga hadi kufikia mwaka 2025 iweze kufikia shule zaidi ya 5000 nchini na watoto Milioni 1.6 ambapo kwa sasa ni watoto Milioni 1 tu ndio wanapata maziwa wawapo shuleni. 

Dkt. Msalya ameendelea kueleza kuwa TDB kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Gain pamoja na Kiwanda cha kusindika maziwa cha Galaxy Food and Beverages Ltd imeweza kuzalisha bidhaa ya maziwa yenye virutubisho iitwayo mtindi laini ulioongezwa virutubisho ambayo haikuwahi kuwepo sokoni tangu kuanzishwa kwa nchi hii. 

Aidha, Dkt. Msalya ameeleza kuwa lengo la kuanzishwa kwa bidhaa hiyo nikuwezesha watoto kuepukana na hali ya Udumavu na Utapiamlo kwani maziwa hayo yanavirutubishi muhimu kwa afya ya watoto. 

Mpango wa Uhamasishaji Unywaji Maziwa Shuleni kwa Mkoa wa Dar Es Salaam umefanyika kwa mara ya kwanza ambapo zaidi ya wanafunzi wapatao elfu nne waliweza kupewa maziwa yalioongezewa virutubisho muhimu kwa ajili ya kuboresha afya zao.