HEIFER INTERNATIONAL YATAKA USHIRIKIANO KUIMARISHA SEKTA YA MAZIWA NCHINI 
                                
                                
                                              
                            
   
                         
                            Mkurugenzi Mkazi wa Heifer International Tanzania, Bw. Mark Tsoxo, ametoa wito kwa wadau wa sekta ya maziwa nchini kuimarisha ushirikiano ili kuongeza tija na uendelevu wa uzalishaji wa maziwa, hasa kwa wakulima wadogo.
Akizungumza katika Kongamano la Wadau wa Maziwa Mkoa wa Geita, Bw. Tsoxo alisema taasisi ya Heifer International imejipanga kuendelea kusaidia wakulima kupitia mafunzo ya ufugaji bora, afya ya mifugo na mbinu za kuongeza thamani ya maziwa, sambamba na kuwaunganisha na masoko ya uhakika.
“Heifer itaendelea kuwekeza kwa wakulima wadogo kupitia mafunzo, utetezi wa sera, na kuunganisha watoa huduma ili tasnia ya maziwa iwe endelevu na kufunguka kwa fursa kwa familia nyingi,” alisema.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza programu za maziwa mashuleni ili kuboresha lishe ya watoto na kukuza matumizi ya maziwa nchini, akibainisha kuwa mipango hiyo pia inasaidia kuongeza soko la maziwa kwa wakulima wa ndani.
Bw. Tsoxo alieleza kuwa mafanikio ya sekta ya maziwa hayawezi kupatikana bila ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, mashirika ya maendeleo na wakulima wenyewe, huku akihimiza kuwepo kwa sera na mazingira bora ya biashara yatakayowawezesha wazalishaji kupata pembejeo, mitaji na masoko.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya maziwa wakiwemo wawakilishi wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), viongozi wa serikali, vyama vya ushirika, na kampuni za usindikaji maziwa.
 
            