IMALINYI KUFUNGUA UKURASA MPYA WA LISHE BORA KWA WANAFUNZI KUPITIA UNYWAJI MAZIWA SHULENI
Shule ya Msingi Imalinyi, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, imeanza maandalizi ya kuanzisha Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni kupitia Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), kwa kushirikiana na Kamati ya Shule, wazazi na viongozi wa Serikali ya Kijiji, kwa lengo la kuboresha lishe ya wanafunzi kwa kuongeza maziwa katika mlo wao, kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP).
Akizungumza katika kikao hicho Kwa niaba ya Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Meneja Masoko wa TDB, Bw. Joseph Semu, alieleza umuhimu wa kuwajumuisha wazazi na jamii katika maandalizi ya mpango huo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maziwa kama sehemu ya mlo wao na kunufaika na lishe bora.
Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Mkoa, Bw. Nicolaus Buji, alieleza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kuhakikisha upatikanaji wa maziwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo na kuendeleza uzalishaji wa maziwa katika eneo hilo.
Naye Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe, Bw. John Deus, alisisitiza umuhimu wa maziwa katika lishe ya watoto na kuhimiza wazazi kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuboresha lishe ya wanafunzi kupitia mpango huo.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Kend’s Milk, Bw. God Nungwi, ambaye ni msindikaji wa maziwa, alieleza kuwa wasindikaji wana nafasi muhimu katika kufanikisha Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata maziwa bora na salama kwa wakati.
Alisema ushirikiano kati ya wasindikaji, shule, wazazi na Serikali ni muhimu katika kuweka utaratibu endelevu wa upatikanaji wa maziwa shuleni, huku ukichochea soko la baadaye la maziwa na kuongeza fursa za biashara kwa wazalishaji na wasindikaji.
Kupitia C-SDTP, TDB inaendelea kushirikiana na shule, wazazi, Serikali za Vijiji na Mitaa pamoja na wasindikaji kuhamasisha uanzishwaji wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni, unaolenga kuboresha lishe ya wanafunzi na kukuza matumizi ya maziwa yanayozalishwa nchini.
