KAIMU MSAJILI WA TDB ASISITIZA ULAJI NA UZALISHAJI WA MAZIWA

Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Bi. Deorinidei Mng’ong’o ametoa maagizo kwa wadau wote wa sekta ya maziwa nchini ili kuimarisha uzalishaji, usambazaji na ulaji wa maziwa, akisisitiza hasa umuhimu wa unywaji wa maziwa shuleni.
Akihutubia wajumbe wa kongamano hilo lililofanyika mkoani Geita Septemba 23, 2025 Kaimu Msajili alisema kuwa maziwa ni chakula cha lishe bora kinachochangia ukuaji wa mwili, afya njema, na maendeleo ya akili kwa watoto.
“Sekta ya maziwa ni uti wa mgongo wa afya na uchumi wa taifa letu. Watoto wanapopata maziwa shuleni, tunajenga kizazi chenye afya bora, akili timamu na nguvu kazi yenye tija,” alisema.
Kaimu Msajili alibainisha kuwa Tanzania huzalisha takribani lita bilioni 3.9 za maziwa kwa mwaka, lakini wastani wa unywaji kwa mtu mmoja bado ni lita 68, chini ya kiwango cha lita 200 kilichopendekezwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO).
Aliweka wazi changamoto zinazokwamisha sekta: mifugo yenye tija ndogo, ukosefu wa miundombinu bora ya ukusanyaji na ubaridi, uelewa mdogo wa jamii kuhusu maziwa, na upungufu wa uwekezaji katika uchakataji vijijini.
Aidha alitoa wito kwa wafugaji kuboresha mbinu za ufugaji, lishe na huduma za afya ya mifugo ili kuongeza uzalishaji wa maziwa sambasamba na kuwataka walimu na wazazi kuhakikisha watoto wanapata maziwa angalau mara moja kwa siku shuleni.
Kongamano hilo pia lilijadili mbinu za kuboresha mnyororo wa thamani wa maziwa, kuhakikisha maziwa yanapatikana kwa wingi, ubora na usalama. Kaimu Msajili aliwataka wadau kushirikiana kwa karibu na Bodi ya Maziwa Tanzania ili sekta hiyo iwe endelevu na yenye tija.
“Hili kongamano lisibaki kwenye maneno tu; tunataka utekelezaji wa maazimio unaoonekana na wenye tija kwa wananchi,” alisema Kaimu Msajili.
Aliahidi Bodi ya Maziwa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha malengo ya Unywaji wa Maziwa Shuleni na uzalishaji endelevu wa maziwa yanafanikiwa.