Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
MAZIWA HAYAPASWI KUWA KINYWAJI CHA ANASA-MNYETI 
04 Jun, 2024
MAZIWA HAYAPASWI KUWA KINYWAJI CHA ANASA-MNYETI 

◼️ TDB mbioni kuanzisha "Bar" ya maziwa 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti ameitaka Bodi ya Maziwa kuhakikisha maziwa yanayosindikwa nchini yanauzwa kwa bei ambayo Watanzania wengi wataimudu badala ya gharama kubwa iliyopo hivi sasa hali inayofanya kinywaji hicho kionekane ni kinywaji cha Anasa pale mtu anapotumia.

Mhe. Mnyeti amesema hayo Juni 01, 2024 kwenye kilele cha Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Unywaji Maziwa duniani yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Furahisha mkoani Mwanza.

"Nchi yetu inakabiliana na changamoto kubwa ya Udumavu ambao kwa kiasi kikubwa unatokana na ukosefu wa virutubisho muhimu mwilini lakini bahati mbaya hivi sasa maziwa yamegeuka kuwa ni starehe na Watanzania hatuna utamaduni wa kunywa kwa sababu tunaona ni kinywaji cha starehe na anayekunywa mbele za watu anaonekana kama ana dharau hivi kwa wale wanaomuangalia" Ameongeza Mhe. Mnyeti.

Akiwa kwenye ukaguzi wa mabanda ya Taasisi zilizoshiriki maonesho ya mwaka huu, Mhe. Mnyeti amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayesimamia sekta ya Mifugo Prof. Daniel Mushi kuzungumza na wasindikaji wa bidhaa hiyo kuhusu vifungashio salama na rafiki na vya bei nafuu ili kupunguza gharama ya maziwa kwa mtumiaji wa mwisho.

"Bei ya Maziwa ipo juu na inawezekana ndio sababu ya kuwafanya wasinywe kwa wingi kama tunavyotegemea kwa sababu leo unamwambia mtoto anunue maziwa kwa gharama ya shilingi 2000 kwa lita moja na kuna kopo ndogo kabisa inauzwa shilingi 700 ambayo naamini kuna baadhi ya kaya tulizonazo hela hiyo ni gharama ya mboga kwa siku nzima hivyo tumegeuza bidhaa hiyo kuwa maalum kwa watu wenye uwezo tu" Amesisitiza Mhe. Mnyeti.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya amebainisha kuwa katika hatua ya kuendelea kuhamasisha matumizi ya Maziwa kwa watanzania, wanakusudia kuanzisha "bar" za maziwa ili kufanya matumizi ya kinywaji hicho kupatikana wakati wote na katika ujazo ambao mteja anaweza kulipia.

"Tulianza na ATM za maziwa kwa majaribio na sasa tutaziongeza ili ziwe nyingi jambo ambalo tunaamini litampa fursa mtu yoyote kupata maziwa wakati wowote anaohitaji" Ameongeza Prof. Msalya.

Akibainisha matukio yaliyofanyika wakati wa Maadhimisho hayo, Prof. Msalya amesema kuwa walitembelea kwenye baadhi ya shule, hospitali na vituo vya watoto wenye mahitaji maalum ili kuhamasisha matumizi ya bidhaa hiyo kwa makundi hayo.

"Lakini kwa mwaka huu tunaenda mbali zaidi ambapo wataalam wetu watabaki hapa kutoa elimu kwa Chama cha Walemavu cha mkoa wa Mwanza  ili wakafanye biashara kupitia bidhaa hii ya maziwa" amesema Prof. Msalya.

Aidha Prof. Msalya amesema kuwa katika kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwenye Maadhimisho ya mwaka jana,  Bodi yake kwa kushirikiana na kiwanda cha Maziwa cha Kilimanjaro wametengeneza maziwa ya mgando yatakayopatikana kwa gharama ya shilingi 500 pekee jambo ambalo litawapa nafasi watu wengi zaidi kutumia bidhaa hiyo.

Maadhimisho ya Wiki ya maziwa mwaka huu yalihudhuriwa na takribani  watu 5000 ambao walifika kwenye mabanda mbalimbali yaliyokuwepo kwenye viwanja vya Furahisha ili kupata elimu kuhusiana na bidhaa ya maziwa.