Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
MTWARA YAHAMASISHWA UMUHIMU WA UNYWAJI MAZIWA SHULENI
24 Sep, 2024
MTWARA YAHAMASISHWA UMUHIMU WA UNYWAJI MAZIWA SHULENI

Bodi ya Maziwa Tanzania imetoa elimu juu ya umuhimu wa unywaji Maziwa pamoja na kugawa Maziwa Kwa wanafunzi wenye uhitaji maalumu kutoka katika Shule mbalimbali zilizopo Manispaa ya Mtwara Mikindani Mkoani Mtwara.

Elimu hiyo imetolewa  Septemba 23, 2024  na Kaimu Mkuu wa Idara ya Ufundi Maziwa Bi. Deorinidei Mng'ong'o akimwakilisha Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania  wakati wa Mkutano  na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano katika Ofisi ya  Mkuu wa Mkoa wa Mtwara

Akiongea kwenye Mkutano huo, Bi. Deorinidei amebainisha umuhimu wa unywaji Maziwa Kwa wanafunzi kuwa huwasaidia katika ukuaji wa akili, kuupa mwili nguvu pamoja nakutunza kumbukumbu ikizingatia kuwa wanafunzi wako katika rika linalohitaji virutubisho vya kutosha katika miili yao.

Ametoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika tukio hilo linalotarajiwa kufanyika siku ya Jumatano Septemba 25, Katika viwanja vya Shule ya Msingi Msufini

Kwa upande wake Daktari wa Mifugo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Dkt. Subira Sendei amesema hali ya Unywaji Maziwa Kwa Mkoa wa huo sio mzuri kutokana na kuwa na Ng'ombe wachache wa Maziwa hivyo hutegemea Maziwa kutoka nje ya Mkoa wa Mtwara.

Aidha ameishukuru Bodi ya Maziwa Tanzania kwakuchagua kuja kufanya uhamasishaji wa Unywaji Maziwa Shuleni ikiwa pamoja na Kongamano la Wadau wa Sekta ya Maziwa nchini katika Mkoa huo kwani kutawafanya wananchi kujifunza na kuingia kwenye ufugaji uliobora.

Naye Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Mtwara Mwl. Zubeda Makame ametoa rai Kwa wazazi wa Mkoa wa Mtwara kuhamasika katika kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika programu hii ya Unywaji wa Maziwa Shuleni kwani Maziwa yanamanufaa mengi kwenye ukuaji wa mtoto kuliko wanavyotumia vyakula vingine ambavyo havina faida yoyote katika ukuaji wao wawapo Shuleni.

Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni huadhimishwa Kila Jumatano ya Mwezi Septemba Kila mwaka ambapo Kwa mwaka 2024 itaadhimishwa  Kitaifa Mkoani Mtwara.