Prof. MASANYIWA AWAASA TDB KUFANYA KAZI KWA BIDII
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Maziwa Tanzania Profesa Zacharia Masanyiwa amewaasa watumishi wa Bodi ya Maziwa Tanzania kufanyakazi kwa bidii kuelekea katika kipindi cha mpito wakati bodi ikiunganishwa na kuwa Taasisi nyingine kubwa ya kusimamia Mazao ya Mifugo hapa nchini.
Prof. Masanyiwa ameyasema hayo Mei 8, 2024 katika kikao cha watumishi wa bodi hiyo kilichofanyika katika Ofisi ya Makao Makuu Dodoma kikichokuwa na lengo la kuwaaga na kuwatakia majukumu mema katika taasisi mpya itakayoundwa hivi karibuni.
"Nataka niwatie faraja kuwa taasisi yetu haijafutwa badala yake tumeunganishwa ili kuundwa taasisi kubwa zaidi itayoongezewa majukumu katika utendaji wa kazi ambapo itashughulika na mazao yote ya mifugo hapa nchini" Amesema Prof Masanyiwa
Vilevile amewataka watumishi wa bodi kila mmoja katika nafasi aliyonayo kuendelea kuongeza ufanisi wa kazi hasa katika kipindi hiki cha mpito kwani kwa sasa jicho la serikali linamulika zaidi ilikupata watumishi watakaoendelea kutumika na taasisi hiyo mpya itakayoanza kazi hivi karibuni.
Bodi ya Maziwa Tanzania iliyoundwa kwa sheria ya Maziwa sura ya 262 ya mwaka 2004 inatarajiwa kuunganishwa na Bodi ya Nyama na kuundwa taasisi mpya itakayoshughulikia mazao ya Mifugo kufuatia serikali kuunganisha baadhi ya taasisi zake ili kuongeza ufanisi.