Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
Prof. Msalya: TUZO YA NANENANE 2024 IWE CHACHU YA URASIMISHAJI TASNIA YA MAZIWA NCHINI 
10 Aug, 2024
Prof. Msalya: TUZO YA NANENANE 2024 IWE CHACHU YA URASIMISHAJI TASNIA YA MAZIWA NCHINI 

Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Prof. George Msalya amewataka wadau wa maziwa kote nchini kuwa chachu ya mabadiliko katika azima ya serikali ya kurasimisha Tasnia ya Maziwa hapa nchini. 

Prof Msalya ameyasema hayo Agosti 9, 2024 baada ya kupokea tuzo ya Mshindi wa Kwanza katika kundi la Bodi za Serikali iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akihitimisha Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo na Mifugo (Nanenane) 2024 yaliyofanyika katika viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma. 

"Nipende kuwaambia wadau wa maziwa hapa nchini, tuzo hii tuliyopewa na Mheshimiwa Rais ikachochee kasi ya kurasimisha Tasnia ya Maziwa hapa nchini, hii ndio itakuwa zawadi pekee ambayo tunaweza kurudisha shukrani kwa Mama yetu na Rais wa nchi yetu" amesema Prof. Msalya 

Akiongea kwa niaba ya Menejimenti ya TDB amewapongeza wafanyakazi wote kwa ushirikiano waliouonesha wakati wote wa maandalizi wa maonesho haya kwani ubunifu na juhudi walizozionesha wakati wa kutoa elimu na huduma kwa wananchi waliokuwa wanatembelea Banda la TDB umechangia kwa kiasi kikubwa kupata tuzo hii. 

"Kupata tuzo hii imedhihirisha kwamba tukijituma na kila mtu akifanya kazi kwa sehemu yake kwa juhudi na maarifa tunaweza kufika mbali zaidi na kuwa Taasisi imara itakayojitosheleza katika kutoa huduma hapa nchini." Ameongezea Prof. Msalya 

Vilevile amewashukuru wadau wote wa maziwa walioshiriki maonesho ya Nanenane kwa Mwaka huu kwani wameongeza nguvu hadi kupata heshima ya kuwa wa Kwanza katika kundi la bodi za mazao hapa nchini, kwani kila mdau kwa namna moja au nyingine amechangia ushindi huu. 

Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo na Mifugo Kitaifa yaliyokuwa yanafanyika Viwanja vya Nzuguni Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 1, 2024 yalihitimishwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Agosti 8, 2024 ambapo Bodi ya Maziwa Tanzania iliibuka Mshindi wa Kwanza katika kundi la Bodi za Serikali kwenye maonesho hayo.