Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
RAS GEITA ATOA MAAGIZO KUIMARISHA UNYWAJI WA MAZIWA SHULENI NA UZALISHAJI WA MAZIWA NCHINI
23 Oct, 2025
RAS GEITA ATOA MAAGIZO KUIMARISHA UNYWAJI WA MAZIWA SHULENI NA UZALISHAJI WA MAZIWA NCHINI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Mohammed Gombati, ametoa maagizo kadhaa kwa watendaji wa serikali na wadau wa sekta ya maziwa nchini, akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka na endelevu katika kuimarisha ulaji na uzalishaji wa maziwa.

Akizungumza wakati wa kongamano la wadau wa tasnia ya maziwa lililofanyika mjini Geita, Bw. Gombati alisema kuwa maziwa ni chanzo muhimu cha lishe bora na maendeleo ya taifa, hivyo ni lazima kila sekta inayohusika ichukue hatua stahiki kuhakikisha Watanzania, hususan watoto wa shule, wanapata maziwa kila siku.

“Tunapaswa kuwekeza katika kizazi chenye afya njema kupitia lishe bora inayojumuisha maziwa. Watoto wanapopata maziwa shuleni, tunajenga taifa lenye akili timamu, afya bora na nguvu kazi yenye tija,” alisema RAS Gombati.


Bw. Gombati amewataka maafisa lishe wa mkoa wa Geita kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu faida za maziwa safi na salama, pamoja na umuhimu wa kuyajumuisha kwenye milo ya kila siku. Alisisitiza kuwa elimu hiyo lazima iwe endelevu na ifikie shule zote, vituo vya afya, na jamii vijijini.

Kadhalika, aliwataka walimu na wazazi kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata maziwa wakiwa shuleni, akisema kuwa programu ya unywaji wa maziwa shuleni ni nyenzo muhimu katika kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.

“Elimu bora inahitaji afya bora — na afya bora inajengwa kwa lishe bora. Walimu na wazazi wanapaswa kushirikiana kuhakikisha watoto wetu hawakosi maziwa shuleni,” alisisitiza.


Katika maagizo yake kwa maafisa mifugo, RAS Gombati aliwataka wahakikishe wanaendelea kuhamasisha wafugaji kufuga kisasa na kutumia teknolojia bora za uzalishaji ili kuongeza upatikanaji wa maziwa mwaka mzima. Alisema kuwa changamoto ya upungufu wa maziwa hasa wakati wa kiangazi inaweza kutatuliwa kwa kuongeza ubora wa malisho, huduma za ugani, na matumizi ya mbegu bora za mifugo.

“Wafugaji wetu wanapaswa kuona mifugo yao kama biashara, si kama urithi tu. Tunahitaji maziwa ya kutosha kwa familia na kwa soko la ndani,” aliongeza.


 

]RAS Gombati alitoa wito kwa wadau wote wa sekta ya maziwa wakiwemo wachakataji, wasambazaji, wafugaji, na taasisi za kifedha kushirikiana kwa karibu na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) katika kukuza thamani ya mnyororo wa maziwa. Alisisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuongeza ubora wa bidhaa, ajira, na kipato cha wananchi.

“Hili kongamano lisibaki kwenye maneno tu; tunataka maazimio yenye utekelezaji unaoonekana na wenye tija kwa wananchi,” alisema.


Mkutano huo uliwakutanisha wadau  mbalimbali, wakiwemo Maafisa wa Serikali, Wawakilishi wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Wadau wa Maendeleo, Wamiliki wa Viwanda vya Maziwa, Vyama vya Wafugaji, Maafisa Mifugo, Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Wataalamu wa Lishe. Mjadala ulilenga kuimarisha sera, ubora wa maziwa, na kuendeleza kampeni ya Unywaji wa Maziwa Shuleni kama sehemu ya mkakati wa taifa wa lishe bora.

Kwa kauli moja, wadau walikubaliana kuunga mkono maagizo yaliyotolewa na RAS Gombati, wakiahidi kushirikiana katika kuhakikisha Mkoa wa Geita na Tanzania kwa ujumla unakuwa mfano wa mafanikio katika sekta ya maziwa.