RC MTANDA AZINDUA WIKI YA MAZIWA KITAIFA, AWATAKA WANANCHI KUNYWA MAZIWA SALAMA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wananchi wa Mkoa huo na kote nchini kunywa Maziwa yaliyosindikwa ili kujihakikishia usalama na ubora wa bidhaa wanayotumia kwa ajili ya kujenga jamii yenye afya.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo Mei 29, 2024 wakati akizindua Maadhimisho ya 27 ya wiki ya Maziwa Kitaifa yanayofanyika kwenye viwanja vya Furahisha Ilemela - Mwanza huku kilele chake kikitarajiwa kuwa tarehe 01 Juni, 2024.
Amesema, kwa wastani mtanzania anakunywa lita 67.5 kwa mwaka wakati malengo ya kidunia ni kunywa lita 200 kwa siku na kwa Mwanza kuna ng'ombe 16,223 ambapo ni wastani wa lita elfu 85 kwa siku ambapo kwa ujumla ni kiasi kidogo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutumia maziwa yalitosindikwa na wazawa ndani ya mkoa ili kukuza uchumi wa wale wote wanaojihusisha na uzalishaji ndani ya Mkoa wa Mwanza na kujijengea utamaduni wa kunywa glasi moja ya maziwa kwa siku.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri Prof. Zacharia Masanyiwa ametumia jukwaa hilo kuwaalika wafugaji kwenye viwanja hivyo ili kujifunza usindikaji na kuboresha mnyororo wa thamani kwani kwa sasa sekta hiyo ina mchango mdogo kwenye Pato la Taifa yaani kwa asilimia 2 tu.
Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya amesmea kuwa Maziwa ni mlo kamili unaojitosheleza kwa kuwa na virutubisho vyote kama vile Madini na Vitamini na kwamba wananchi wana kila sababu kuyanywa.
Aidha, amebainisha mchango wa sekta hiyo kwenye ajira kwani kaya milioni 2.2 nchini zinajihusisha na uzalishaji na kuajiri watu na kwamba wadau zaidi ya Elfu 7 wanajihusisha kwenye mnyororo wa thamani.
Maadhimisho hayo ya Kitaifa kwa Mwaka 2024 yanaenda sambamba na kauli mbiu isemayo; 'Kunywa Maziwa Salama kwa Afya Bora na Uchumi Endelevu.'