TDB YAHIMIZWA KUENDELEA KUSAJILI WADAU WA TASNIA YA MAZIWA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Ndg. Abdul Mhinte ameihimiza Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) kuendelea kuwatambua na kuwasajili wadau wa Tasnia ya Maziwa ili kuongeza Uzalishaji wa maziwa nchini.
Ndg. Mhinte amesema hayo wakati akizungumza na Watumishi wa TDB katika Kikao kazi kinachofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Aprili 16, 2025.
"kama wadau wa Tasnia ya Maziwa hawafahamiki na hawajasajiliwa, ni ngumu sana kufikia Malengo na kuzalisha Maziwa kwa wingi, kwani wanahitaji kutatuliwa changamoto zao, ikiwemo za Masoko ya Maziwa hayo" amesema Ndg. Mhinte
Vilevile, Ndg. Mhinte amesema kuwa wadau wa Tasnia ya Maziwa wapo sehemu mbalimbali nchini, na ni vyema Vituo vya ukusanyaji Maziwa vikarekebishwa na kuongezwa, ikiwa pamoja na Usimamizi mzuri ili Maziwa yakusanywe kwa wingi.
Ndg. Mhinte, pia amehimiza Bodi kubuni Miradi mbalimbali kama ya Bar za Maziwa ili kuhakikisha Watumishi wanayapata kiurahisi na kuongeza Pato la Taifa.
Naye, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Prof. George Msalya amesema kuwa leo wamekuwa na Kikao na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kujadili Maendeleo ya Taasisi yao hususani Maendeleo ya Tasnia ya Maziwa hapa nchini pamoja na utendaji kiujumla.
"tumepokea maagizo yote tuliopewa na Naibu Katibu Mkuu ambayo yatatujenga na kuongeza hali ya utendaji kazi katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku katika Tasnia ya Maziwa" amesema Prof. Msalya
Halikadhalika, Prof. Msalya amesema kwa sasa Maziwa yanakusanywa katika vituo 258 maalum vya kukusanyia, na wataendelea kuongeza vituo vingine pamoja na Miradi mingine kama Bar za Maziwa ili kuhakikisha Maziwa yanapatikana kwa wingi nchini.
Prof. Msalya amebainisha kuwa kwa sasa Takwimu zinaonyesha kila Mtanzania mmoja anatumia takribani Lita 67.5 kwa mwaka, ila viwango vilivyowekwa Kimataifa kwa mtu mmoja kunywa Maziwa kwa mwaka ni Lita 200.