TDB YAKUTANA NA WACHUUZI WA MAZIWA WILAYA YA CHALINZE
Bodi ya Maziwa Tanzania kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze imekutana na wauzaji na wasafirishaji wa maziwa wilayani hapo wakati wa oparesheni wa kufanya ukaguzi wa maziwa kwa lengo lakujionea hali halisi ya namna wachuuzi hao wanavyosafirisha maziwa hayo kufika sokoni.
Opereshi hiyo iliyodumu kwa muda wa siku mbili wilayani hapo kuanzia Mei 15 hadi Mei 16 2024 imebaini baadhi ya wachuuzi wa maziwa wasiofuata sheria na kanuni za usafirishaji maziwa ambapo wengi wao wamekuwa wakitumia magari yasiyokuwa na vigezo vya kusafirishia bidhaa hiyo badala yakutumia magari yenye ubaridi yaliyoruhusiwa kisheria kubebea bidhaa hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wachuuzi hao wamesema kuwa inawalazimu kutumia njia hiyo kwani magari yanayotakiwa kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa hiyo ni ghali hivyo kushindwa kumudu gharama zake ukilinganisha na usafiri wa pikipiki na magari ya abiria wanayotumia.
"Kwa siku moja tunauwezo wa kukusanya na kusafirisha maziwa zaidi ya lita 4000 kwenda jijini Dar es Salaam ambako ndio soko kubwa la maziwa lilipo, tunaomba kama serikali itatusaidia kutupatia gari la ubaridi kwa gharama nafuu tutaweza kumudu gharama hizo kwani biashara yetu huwa ni ya msimu wakati wa uzalishaji wa maziwa ukiwa kwa wingi" wamesema baadhi ya wachuuzi wa maziwa.
Kwa upande wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Mtekinolojia wa Chakula wa bodi hiyo Bi. Neema Moshi baada ya kufanya ukaguzi katika maeneo ya kukusanya na kusindika Maziwa alitoa elimu juu ya usafirishaji sahihi wa maziwa na namna ya kusindika maziwa kitaalamu tofauti na wanavyotumia njia za kienyeji kusindika bidhaa hiyo.