Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
TDB YASISITIZA MPANGO WA UNYWAJI MAZIWA SHULENI KUBORESHA AFYA NA UTENDAJI WA WANAFUNZI
24 Oct, 2025
TDB YASISITIZA MPANGO WA UNYWAJI MAZIWA SHULENI KUBORESHA AFYA NA UTENDAJI WA WANAFUNZI

Bodi ya Maziwa Tanzania imesisitiza Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni ili kuboresha Afya na Utendaji wa Wanafunzi wakiwa shuleni.

Hayo yamesemwa na Meneja Masoko wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Bw. Joseph Semu wakati akiwasilisha mada ya umuhimu wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni katika kongamano la wadau wa maziwa lililofanyika mkoani Geita Septemba 23, 2025.

Akizungumza na  wajumbe wa Kongamano hilo, Bw. Semu amesema mpango huu unalenga kuongeza unywaji wa maziwa miongoni mwa wanafunzi, hatua inayosaidia kuboresha lishe, afya, na utendaji wa watoto shuleni. “Tunataka kila mtoto nchini apate fursa ya kunywa maziwa ya kutosha kila siku ili kuimarisha ukuaji na afya yake kwa ujumla,” amesema Bw. Semu.

Bw. Semu aliongeza kuwa Bodi ya Maziwa Tanzania inashirikiana na shule, wazazi, na wazalishaji wa maziwa ili kuhakikisha upatikanaji wa maziwa kwa uhakika. Mpango huu pia unachangia kuongeza uelewa wa umuhimu wa lishe bora katika maendeleo ya watoto na kupunguza tatizo la utapiamlo.

Aidha, ameitaka jamii kuunga mkono mpango huu kwa kuhakikisha maziwa yanapatikana kwa urahisi kwa shule zote, huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa wadau wote ni ufunguo wa mafanikio.

Kongamano la wadau wa maziwa Geita limeendelea kujadili njia za kuboresha sekta ya maziwa nchini, na Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni umepata mkono mkubwa kutokana na faida zake kwa afya ya watoto na maendeleo ya elimu.