Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
TDB YATAKIWA KUTATUA CHANGAMOTO YA BEI YA MAZIWA NCHINI
04 Jun, 2024
TDB YATAKIWA KUTATUA CHANGAMOTO YA BEI YA MAZIWA NCHINI

Ili kuondokana na changamoto ya udumavu nchini pamoja na wananchi kutokunywa maziwa Bodi ya Maziwa Tanzania(TDB) imetakiwa kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo suala la kupunguza bei ya maziwa ambayo ipo juu ili watanzania waweze kumudu gharama hizo na kufika malengo ya kitaifa ya kila mtu kunywa lita 200 kwa mwaka. 

Pia TDB imetakiwa kushughulikia suala la vifungashio ambalo limeezwa kuwa ni moja ya sababu inayochangia gharama ya maziwa kuwa juu huku wasindikaji na watengenezaji wa bidhaa hiyo wametakiwa kuwa tayari kupunguza bei ya maziwa. 

Agizo hilo limetolewa Juni 1,2024 na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti, wakati akifunga maadhimisho ya 27 ya wiki ya maziwa kitaifa yanayofanyika kitaifa mkoani Mwanza katika uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani hapa yenye kauli mbiu “Kunywa maziwa salama kwa afya bora na uchumi endelevu ikiwa ni siku maalumu ya unywaji maziwa duniani. 

Mnyeti ameeleza kuwa kuna tatizo la udumavu nchini linalotokana na watoto kutopata virutubisho bora na unapo komaa mtoto anakosa akili hivyo tunatengeneza taifa la watoto wasiokuwa na akili na tafsiri yake ni kwamba baadae halitakuwa na maprofesa, madaktari. 

Hivyo ameitaka Bodi ya Maziwa Tanzania kujadili kwa kina waone namna ya kulitatua jambo hilo kwa sababu kinachopatikana kwenye maziwa na mtoto wa kitanzania akifanikiwa kunywa maziwa angalau lita moja kwa wiki ni suluhisho tosha la udumavu nchini.
Ambapo ameeleza kuwa leo maziwa yanaonekana kama kinywaji cha anasa,kwamba anayekunywa maziwa ni anayefanya starehe,”maziwa yamegeuka kuwa starehe ,maana Watanzania hatuna utaratibu wa kunywa maziwa kwa sababu maziwa ni starehe,tunako kwenda kwenye kizazi kitakachokuja itakuwa ni hatari sana bei ya maziwa ipo juu inawezekana ndio sababu ya Watanzania hawanywi maziwa,”. 

“Mwenyekiti wa Bodi naomba hili mlifanyie kazi leo unamwambia mtoto anunue maziwa kwa shilingi 2,000, 4,000 kwa lita moja, shilingi 1,500 kwa nusu lita, shilingi 700 kwa milimita,ni nani?, ni wangapi?,wapo wapi?, wanaweza kununua kale kakopo kadogo kwa shilingi 700,wakamudu haiwezekani,zipo familia nina uhakika shilingi 700 ni mboga ya siku nzima,”ameeleza Mnyeti na kuongeza kuwa; 

“Sasa ni familia gani inaweza kutoa shilingi 700 kumpa mtoto wake akanunue kopo dogo la maziwa halafu anywe pekee ake ambapo hata hivyo mtoto hawezi kushiba hazipo,kwaio tafsiri yake ni kwamba tumeachia maziwa watu wenye uwezo waendelee kunywa pekee yao halafu hawa wa chini hawanywi maziwa kwa sababu hawana uwezo wa kumudu gharama hizo,”. 

Sanjari na hayo ameiagiza bodi hiyo wakafanyia kazi suala la changamoto ya vifungashio ambalo limekuwa sababu ya gharama za maziwa kuwa juu ili Watanzania wanywe maziwa, vinginevyo yatabaki ya kupigia picha huku akiwashauri wasindikaji wa maziwa kutumia vifungashio vya karatasi vinavyotokana na miti kuepuka kutumia mifuko ya nailoni (plasitiki). 

“Bodi nawaagiza tena nendeni mkalifanyie jambo hili kwa uharaka vifungashio vitokee kufungashwa kwenye lailoni’plastiki’, tuanze kufungasha kwenye karatasi kwa sababu tuna miti mingi kule Iringa na Sengerema, akipatikana mchakataji mzuri na tukapata viwanda vizuri ambavyo vitatengeneza vifungashio hivyo tunaweza kushusha bei ya maziwa,” na kuongeza kuwa; 

“Na nyinyi wasindikaji wa maziwa muwe tayari kushusha bei kwa sababu nilikuwa nauliza maziwa ambayo hayana sukari shilingi ngapi na yenye sukari shilingi ngapi bei ni moja,yenye vanilla na yasiyo na vanilla bei moja inawezekaneje bei moja kwenye kila kitu,sasa na nyie watengenezaji mmeweka bei ambayo imetengeneza ‘gap'(tabaka) kati yenu na wanywaji twende tukafanyie kazi changamoto hizo ili mwakani tupeleke elimu hii kwenye mikoa inayoongoza kwa udumavu nchini,”. 

Aidha ameeleza kuwa serikali imerahisisha ufugaji bora kwa kugawa mbegu za madume bora ya ng’ombe wa kisasa wenye tija, hivyo wafugaji wachangamkie fursa hiyo. 

“Rais Dk. Samia pia ameruhusu benki zitoe mikopo kwa wafugaji, changamkieni mikopo hiyo kama wavuvi walivyokopeshwa vizimba.Msilalamike kopeni fedha zipo,hatutaki ng’ombe wa kuzalisha lita tano za maziwa kwa siku na hatutaki mpeleke mifugo yenu kwenye mashamba ya wananchi, kopeni mfuge kisasa,”amesema. 

Msajili wa Bodi ya Maziwa,Profesa George Msalya amesema kwa miaka ya karibuni wametumia sh.bilioni 23 kuagiza maziwa nje sababu ya mchango mdogo wa tasnia ya maziwa,watazigeuza changamoto kuwa fursa za kukuza na kuongeza mchango katika uchumi wa nchi huku wakifikiria kuja na bar za maziwa na ATM za maziwa ili kuboresha sekta ya maziwa na kuleta tija nchini. 

“Elimu waliyopata wazalishaji na wasindikaji wa maziwa wakaitumie kuongeza mchango katika tasnia kwa kuzalisha maziwa ya unga tuondoe gharama za kuagiza maziwa nje,”amesema. 

Profesa Msalya ameeleza kuwa zaidi ya wananchi 5,000 wamejitokeza kutembelea mabanda kwenye madhimisho hayo lakini pia bodi hiyo imetembelea shule mbalimbali,hospitali,imetia elimu na kugawa maziwa hiyo yote ikiwa ni kuhamasisha unywaji maziwa kwa jamii. 

Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Zacharia Masanyiwa ametoa wito kwa wananchi na wadau wa Mkoa wa Mwanza watumie maarifa, elimu na ujuzi waliopata katika maadhimisho hayo kwa ajili ya maendeleo ya tasnia ya maziwa na kuimarisha uchumi wa kaya nchini. 

“Siku zote nimekuwa nikisisitiza kuwa maziwa ni lishe,ni biashara,ni uchumi pia maziwa ni pesa na tuone kwa namna gani elimu hii tunayoipata itasaidia katika maendeleo ya tasnia,”.