Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
WADAU WA MAZIWA JIJINI MWANZA WATEMBELEA SHAMBA LA MIFUGO
16 Oct, 2023
WADAU WA MAZIWA JIJINI MWANZA WATEMBELEA SHAMBA LA MIFUGO

Bodi ya Maziwa Tanzania kwa kushirikiana na Jukwaa la Wadau wa Maziwa jijini Mwanza imeratibu ziara ya mafunzo ya siku moja kwa Wadau wa maziwa wa mkoa wa Mwanza kutembelea shamba la Mifugo Mabuki lililoko wilayani Misungwi mkoa wa Mwanza ikiwa ni matokeo ya Kongamano la wadau wa Maziwa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni Septemba 27, 2023.

Ziara hiyo imefanyika Octoba 13, 2023 Kwa lengo la kuona na kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanyika katika shamba hilo ili kuongeza maarifa ambayo yatawasaidia katika shughuli zao za ufugaji sanjari na kutambua fursa wanazoweza kunufaika nazo.

Pamoja na ziara hiyo, wadau waliweza kutembelea Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiwemo Kituo cha Shamba la Uzalishaji wa Chakula cha Mifugo (LMU) ambapo waliweza kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika mahali hapo hasa namna ya uzalishaji wa chakula cha mifugo na uhifadhi wake.

Akizungumza na wadau hao, Meneja Msaidizi wa Shamba Bi. Asteria Mwaya aliwasisitiza wafugaji wa Mwanza kujikita katika uwekezaji wa Kilimo cha Mifugo zaidi kuliko kutegemea  machicha yatokanayo viwandani Kama chakula kikuu cha mifugo yao.

Aidha, Bi. Asteria ameahidi kama Taasisi wako tayari kutoa mafunzo ya maandalizi na  utunzaji wa  malisho kwa wakulima pale watakapohitaji kupata mafunzo hayo sambamba na kuuza malisho na mbegu.

Wakati huo huo walitembelea Chuo cha Mifugo (LITA) na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Chuo hicho Bw. Jacob Ngowi ambapo alieleza kuwa shughuli kubwa inayofanyika chuoni hapo ni kutoa mafunzo ya elimu ya Mifugo Kwa wanafunzi na mafunzo ya  ufugaji bora Kwa wafugaji.

Wakiwa chuoni hapo waliweza kupata elimu ya namna ya shughuli za unenepeshaji wa Mifugo zinazofanywa na vijana wa BBT walioko chuoni hapo wakilelewa na kufanya unenepeshaji wa Mifugo Kwa vitendo ili waweze kupata uzoefu hivyo Mkuu wa Chuo aliwasisiza wadau wa Maziwa kutumia fursa hiyo kwani soko linahitaji nyama iliyobora.

Aidha, aliwasisitiza wadau kutumia Wagani wa Mifugo ili kuleta tija katika mnyororo wa thamani wa Mifugo kwani wapo Kwa ajili yao hivyo wafugaji wanapaswa kuwatumia kikamilifu.