WADAU WA MAZIWA MKOANI MWANZA WAPEWA ELIMU KUKUZA BIASHARA NA KUFUATA SHERIA
Wadau wa maziwa mkoani Mwanza wamepewa elimu ya biashara sanjari na kuzingatia sheria za usajili wa biashara na taratibu za kuomba vibali, ili kukuza biashara zao na kufanya biashara yenye tija.
Elimu hiyo imetolewa na Maafisa kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) walipofanya Kikao cha pamoja na wadau wa maziwa mkoani Mwanza hivi karibuni ambapo kwa mwaka 2023/2024 uzalishaji wa maziwa mkoani Mwanza ulifikia lita milioni 398.53, lakini wastani wa asilimia 0.6 tu ya maziwa hayo yalifanyiwa usindikaji kupitia viwanda vidogo vinavyopatikana mkoani humo.
Akiongea kwenye kikao hicho Afisa Sheria Mwandamizi wa TDB Bi. Nice Tibilengwa aliwahimiza wafanyabiashara wa maziwa kuzingatia sheria za usajili ili kuepukana na adhabu zinazoweza kutozwa. “Usajili wa wadau wa maziwa unafanywa kwa mujibu wa Sheria ya Maziwa, Sura 262 ya mwaka 2004, kifungu 17(1) na 17(2), pamoja na kanuni ya usajili ya mwaka 2007 na marekebisho yake ya mwaka 2020 kifungu cha 4(1) na 4(2),” alisema Tibilengwa.
Naye Afisa Masoko kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania, Bw. Hamisi Kiimbi, amewaasa wafanyabiashara hao kuzingatia taratibu za kuomba vibali vya kutoa au kuingiza maziwa nchini, kwani serikali inatoa vibali hivyo ili kulinda afya za walaji na kuweka ukomo wa bidhaa hiyo sokoni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wamajadiliano, Bi. Rehema Mwalugala, mfugaji wa ng'ombe, alieleza kuwa pamoja nakupewa elimu kuhusu ukuzaji wa biashara na kufuata sheria ni muhimu pia wafugaji kupata elimu ya ufugaji bora, kutunza na kulisha wanyama kwa utaratibu mzuri ili kupata maziwa yaliyo bora.
Awali akifungua kikao hicho Afisa Mifugo wa Mkoa Bw. Peter Kasere kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza alieleza kuwa ili kuimarisha Tasnia ya Maziwa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imejielekeza katika kuboresha mazingira ya ufugaji wenye tija, huku ikihakikisha uwekezaji katika viwanda vya kusindika maziwa unakuwa mkubwa.
“Mpaka sasa, Mkoa unajumla ya mashamba makubwa 15 ya ng’ombe wa maziwa na Chama kikubwa cha Ushirika wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa (UWAWAMWA) ambacho kimeanza kuchakata mtindi na yogati. Pia, kuna viwanda vidogo 13 vya kuchakata maziwa,” Alisema Kasere
Kasere aliongeza kuwa jitihada za kuhamasisha kilimo cha malisho bora ya ng'ombe, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, pamoja na kuendeleza uanzishwaji wa kiwanda cha maziwa cha Mabuki, zinaendelea.