Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
Wadau wa Sekta ya Maziwa punguzeni bei ili Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni ufanikiwe : Naibu Waziri Mnyeti
02 Oct, 2023
Wadau wa Sekta ya Maziwa punguzeni bei ili Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni ufanikiwe : Naibu Waziri Mnyeti

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewaomba wadau wa tasnia ya maziwa nchini kupunguza bei ya maziwa ya Shs 1800 kwa nusu lita ili Mpango wa Unywaji Maziwa kwa watoto wote shuleni ufikie malengo.

Kauli hiyo imetolewa Septemba 27, 2023 kwenye viwanja vya Furahisha Mkoani Mwanza na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni Duniani ambapo Kitaifa imefanyika Mkoani humo.

Mhe. Mnyeti amesema Serikali imefuta tozo zote zinazohusu maziwa hivyo mamlaka husika ziangalie bei muafaka eneo la vifungashio ili wadau wa Tasnia hiyo wasiingie gharama kubwa.

"Bado Mkoa kama wa Mwanza unakabiliwa na hali ya udumavu wa watoto hii imechangiwa na ukosefu wa lishe bora, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha unywaji wa maziwa uwe sehemu ya mlo wa mtoto shuleni." amesisitiza Mhe.Mnyeti.

Amesema itakuwa ni kazi bure kuendelea kuhimiza unywaji wa maziwa kila ifikapo kilele cha maadhimisho hayo wakati uwezo wa kumudu gharama hiyo haupo kutoka kwa wazazi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi ameishukuru Wizara kwa kuona umuhimu wa maadhimisho hayo kufanyika Mkoani humo kutokana na miradi mingi ya kuboresha mifugo inatekelezwa kuanzia Shamba la Taifa la Mifugo Mabuki na kwenye baadhi ya wilaya.


"Mhe. mgeni rasmi Serikali ya awamu ya sita imeleta mitamba 500 Mkoani Mwanza kwa ajili ya kuleta tija ya maziwa na nyama kwa wafugaji, pia wapo vijana wanaopatiwa mafunzo maalum ya ufugaji wa kisasa huko Mabuki," Mhe.Makilagi.

"Bado tuna changamoto ya unywaji wa maziwa nchini ambapo hadi sasa mtu mmoja anakunywa lita 62 kwa mwaka wakati kwa mujibu wa mwongozo wa Shirika la Afya la  kimataifa mtu mmoja anatakiwa kunywa lita 200 kwa mwaka, hivyo inahitajika kazi ya ziada kuhamasisha jamii umuhimu wa kunywa maziwa," Dkt.George Msalya,Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini.

Kuelekea kilele hicho Bodi ya Maziwa ilifanya zoezi la ugawaji wa maziwa shuleni na utoaji wa elimu kwa baadhi ya shule Mkoani Mwanza pamoja na kufanya kongamano lililowahusisha wadau wa Tasnia ya Maziwa na walimu.
Kila Jumatano ya mwisho wa Septemba Tanzania inajumuika na Mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha siku ya unywaji maziwa shuleni ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema "Mpe mtoto maziwa kwa maendeleo bora Shuleni"