WALIMU MTWARA WAPIGWA MSASA UMUHIMU WA MAZIWA KWA WATOTO SHULENI
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bi. Nanjiva Nzunda amewataka Walimu na wadau wa sekta ya maziwa mkoani humo kuyatumia maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni kutoa elimu na kuwahamasisha wazazi na walezi kuwapa watoto maziwa ili kuimarisha zao.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bi Bahati Geuzye, kwenye Kongamano la Maendeleo ya Tasnia ya Maziwa Katika Ukumbi wa Boma ulipo katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi Nzunda amesema kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni itakayofanyika Mkoani Mtwara Septemba 25, 2024 mkoa utayatumia kama darasa kuwahamasisha wadau wake kufahamu umuhimu wa maziwa kwa watoto shuleni.
"Sote tunafahamu sehemu kubwa ya familia katika jamii zetu zinakabiliwa na changamoto ya kuwawezesha watoto kupata mlo kamili kabla ya kwenda Shule na hata wanaporejea nyumbani baada ya masomo" Alisema Bi Nzunda.
Kaimu Katibu Tawala Nzunda aliongeza kuwa hali hiyo imekuwa ikichangia kupungua kwa umakini wa kujifunza miongoni mwa Watoto sambamba na kuathiri matokeo ya mitihani yao ya mwisho.
Aidha Kaimu Katibu Tawala Nzunda amewataka wazazi, walezi na walimu kuzingatia kanuni bora za utoaji lishe kwa watoto shuleni ikiwa ni pamoja na kuhakikisha chakula wanachopewa kinajumuisha viini lishe vyote ikiwemo protini, wanga, mafuta, vitamini na madini muhimu.
" Ndugu zangu tumewasikia wataalamu wetu wakitueleza kuwa mtoto akipata glasi moja ya maziwa kwa siku atakuwa amepata lishe bora yenye virutubisho kwa afya yake, hivyo niwaagize walimu na wataalamu mliopo hapa nendeni mkalisimamie hili" Aliongeza Bi Nzunda.
Awali, Kaimu Mkuu wa Idara ya Masoko kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Bw. Joseph semu akiwasilisha mada kwa niaba ya Msajili wa TDB Prof. George Msalya, juu ya hali ya Tasnia ya Maziwa Nchini na Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni amesema kuwa upo umuhimu wa Walimu kuuelewa Mpango huu kwani umeleta mafanikio makubwa kwa mikoa ambayo inatekeleza mpango huo kama kuboresha na kuongeza kiwango cha ufaulu, kuongeza kiwango cha mahudhurio na kupunguza utoro na kujenga kizazi cha watoto wenye afya bora.