Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
WANAFUNZI ZAIDI YA 3000 WANYWA MAZIWA KUBORESHA AFYA GEITA
25 Sep, 2025
WANAFUNZI ZAIDI YA 3000 WANYWA MAZIWA KUBORESHA AFYA GEITA

WANAFUNZI wapatao 3,385 wa Shule za Msingi na Sekondari mkoa wa Geita wamekunywa maziwa kwa ajili ya ustawi wa Afya Bora na Lishe.

Akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni yaliyofanyika Septemba 24, 2025 katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Mkoani hapo, Mwakilishi wa Msajili Bodi ya Maziwa Tanzania, Bi. Deorinidei Mng’ong’o alisema maziwa yaliyotolewa ni Pakti 3964 ambayo ni sawa na lita 1004.6.

Mng’ong’o alisema kabla ya Siku ya kilele kumekuwepo na Matukio kadhaa yaliyokuwa yanaendelea kama vile kutembelea wanafunzi wenye uhitaji maalumu ambapo zaidi ya wanafunzi 3,385 walinufaika kwakupata Maziwa ili kuendelea kuboresha Afya zao.

Alisema idadi ya lita za maziwa zilizotolewa kuanzia Septemba 22 hadi Septemba 24 mwaka huu ni lita 1004.6.

“Maziwa ni mlo kamili hivyo natoa rai kwa Wazazi, Walezi na Walimu kuhakikisha watoto wetu wanapata maziwa kwa lishe bora, Afya nzuri na ukakamavu wa akili”alisema.

Aidha alisema zoezi hili la unywaji wa maziwa ni endelevu kwa nchi nzima, pia anatoa rai kwa wadau wote wenye mapenzi mema kwa watoto kushirikiana na Bodi ya maziwa Tanzania ili kuimarisha afya za watoto.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba ameshukuru Bodi ya maziwa Tanzania kwa kufanyia kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni katika mkoa wa Geita.

Komba aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapatia watoto wao maziwa ili kuondoa udumavu.

Vilevile ameiasa jamii kutotafsiri Maziwa kama bidhaa ya anasa kwenye familia zetu bali ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kuhakikisha Maziwa yanapatikana kwenye familia.

Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni hufanyika kila jumatano ya mwisho wa mwezi Septemba, ambapo Kwa mwaka huu yamedhimishwa Mkoani Geita.