Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
'WATANZANIA TUSHIRIKIANE KUBORESHA AFYA NA LISHE KWA WATOTO WETU' MSAJILI TDB
11 Dec, 2023
'WATANZANIA TUSHIRIKIANE KUBORESHA AFYA NA LISHE KWA WATOTO WETU' MSAJILI TDB

Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Dkt. George Msalya ametoa wito Kwa watanzania hapa nchini kushirikiana na wadau mbalimbali walio katika mnyororo wa thamani wa maziwa ili kuboresha afya na lishe kwa watoto kwa kuwapatia Maziwa wakiwa Shuleni.

 Ameyasema hayo Desemba 7, 2023 wakati akitoa salamu za TDB wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni kwa Mkoa wa Dar es Salaam ulioenda sambamba na utambulisho wa bidhaa mpya ya mtindi laini uliongezewa virutubisho ikiwa na lengo la kupunguza hali ya Udumavu na Utapiamlo hapa nchini.

Katika salamu zake ameelezea kuwa TDB katika kupambana na hali ya Udumavu na Utapiamlo hapa nchini imeweka Mpango jumuishi wa lishe ambapo imepanga hadi kufikia mwaka 2025 iweze kuwafikia shule zaidi ya 5000 nchini.

Naye Afisa Lishe toka Taasisi ya Chakula na Lishe  Tanzania (TFNC)  Ndg. Elois Ghala amesema japokuwa  wastani wa kila mtu wa kunywa maziwa ni lita 200 kwa mwaka ili kumuwezesha kuwa na afya bora lakini tafiti bado zinaonesha  kuwa Watanzania wanakunywa maziwa kwa wastani wa lita 62 tu kwa mwaka hivyo ametoa wito kwa jamii kuwa na desturi ya kunywa maziwa kwa lengo la kuimarisha afya zao hasa kwa watoto.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika tukio hilo Katibu Tawala sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Dkt. Elizabeth Mshote ameeleza kuwa kati ya shule Milioni 1.2 za Mkoa wa Dar es salaam ni shule 8 tu ndizo zinakunywa Maziwa Shuleni hivyo amewataka maafisa lishe, wakuu wa shule na wadau mbalimbali kuweka mikakati ya kuwezesha watoto kupata maziwa wawapo Shuleni.

Uzinduzi wa Uhamasishaji wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni ulioenda sambamba na utambulisho wa bidhaa mpya ya mtindi laini uliongezewa virutubisho kwa Mkoa wa Dar es Salaam umefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ubungo Plaza iliyopo Wilaya ya Ubungo Desemba 7, 2023 ambapo zaidi ya wanafunzi 4,000 walishiriki tukio hilo.