Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
WAZIRI ULEGA AKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA POLAND
19 Jan, 2024
WAZIRI ULEGA AKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA POLAND

Waahidi kuwekeza TZS. Bilioni 175 kwenye Tasnia ya Maziwa

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, Januari 18, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Wawekezaji kutoka Kampuni ya Uwekezaji ya Contractus ya nchini Poland ambao wameonesha nia ya kufanya uwekezaji kwenye Tasnia ya Maziwa hapa nchini. 

Wawekezaji hao ambao ni Makamu Mwenyekiti wa Kampuni Contractus, Bw. Witold Karczewski na Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara ya Poland ambaye pia ni Meneja Mauzo wa Kampuni, Bw. Adam Borawski wameonesha nia ya kuingia ubia na Serikali ya Tanzania Kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuleta teknolojia ya kisasa ya kupoza maziwa katika vituo mbalimbali vya kukusanyia maziwa nchini. 

Nia yao kuanzia mwaka 2024/ 2025 kuanza uwekezaji huo ambapo wataanza na vituo 500 nchi nzima vyenye uwezo wa kukusanya kati ya lita 2000 hadi 6000 kwa siku. Uwekezaji huo unatarajiwa  kuongeza ukusanyaji wa lita takribani milioni moja za maziwa kwa siku hapa nchini. 

Aidha, mpango huo unaotarajiwa kuwa wa miaka 2 unakadiriwa kugharimu TZS. Bilioni 175, na inakusudiwa kupata ufadhili kutoka kwa Wadau na Serikali ya Poland.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahakikishia wawekezaji hao ushirikiano wa kutosha ili mradi huo uweze kuanza haraka ili tasnia ya maziwa iweze kuwa na tija zaidi kwa taifa. 

Kampuni hiyo ya Contractus inatengeneza na kuuza Machine/Vifaa vya Kukusanyia maziwa ambazo zinatumia umeme wa jua na wana uzoefu wa kufanya kazi katika Tasnia ya Maziwa hususan usambazaji wa mashine na vifaa vya kukusanyia na kusindika maziwa kwa miaka 35 katika nchi mbalimbali ikiwemo nchi za Ulaya, Asia, na Afrika.  Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe na Msajili wa Bodi ya Maziwa, Prof. George Msalya.