Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAFANIKISHA KUINUA KIWANGO CHA UZALISHAJI MAZIWA NCHINI
28 Mar, 2024
WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAFANIKISHA KUINUA KIWANGO CHA UZALISHAJI MAZIWA NCHINI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi yake ya Bodi ya Maziwa Tanzania imefanikisha kuinua kiwango cha uzalishaji wa maziwa hapa nchini kutoka lita Bilioni 2.2 mwaka 2020/21 hadi kufikia lita Bilioni 3.6 mwaka 2022/23. 

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Mifugo Profesa Daniel Mushi wakati akifungua Mkutano wa Usambazaji wa Nakala za Mpangokazi wa Utekelezaji wa Programu ya Unywaji Maziwa Shuleni pamoja na makabidhiano wa vibanda vitakavyotoa huduma ya maziwa shuleni uliofanyika Machi 27, 2024 katika ukumbi wa OSHA mkoani Dodoma. 

Katika hotuba yake amesema kuwa jitihada kubwa zimefanywa na serikali katika kuhakikisha uzalishaji, uchakataji na upatikanaji wa mazao ya mifugo nchini ikiwemo maziwa unaongezeka ambapo imeboresha kosaafu za mifugo kwa njia ya uhimilishaji, ununuzi wa madume bora ya mbegu na ununuzi wa ng'ombe wazazi 3,160 katika mashamba ya serikali, ikiwemo mashamba ya kuzalisha mitamba ya ng'ombe wa maziwa na udhibiti wa magonjwa ya mifugo nchini.


Aidha, ameendelea kuongeza kuwa pamoja na ongezeko kubwa la uzalishaji wa mazao ya mifugo ikiwemo maziwa, takwimu zinaonesha kuwa ulaji wa vyakula vyenye asili ya wanyama ni wa kiwango cha chini hapa nchini, mathalani ametolea mfano kiwango cha unywaji maziwa kwa mtu kwa mwaka ni lita 62, ukilinganisha na kiasi kinachopendekezwa cha lita 200 kwa mtu kwa mwaka kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), hivyo kwa kuona hayo wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa Mpangokazi wa Utekelezaji wa Programu ya Unywaji Maziwa Shuleni kama njia moja wapo ya kuongeza unywaji wa maziwa nchini. 

Awali, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Prof. George Msalya akitoa maelezo ya jumla kuhusu mchakato mzima wa uandaaji na yaliyomo ndani ya Mpangokazi huo amesema kuwa maandalizi ya Mpangokazi wa Unywaji Maziwa Shuleni umezingatia ushiriki na ushirikishwaji wa wadau kwa kufanya vikao mbalimbali vilivyojadili na kupokea maoni ya wadau, kupata uzoefu kwa wanaotekeleza programu kama hii ndani na nje ya nchi. 

Naye Ndugu Patrick Codjia, Mkuu wa Masuala ya Lishe kutoka UNICEF akitoa salamu za Shirika hilo amesema kuwa usambazaji wa Mpangokazi huo ni hatua muhimu ya utekelezaji wa Mpangokazi Jumuishi wa Lishe Kitaifa ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka viashiria vyakuhakikisha mazao ya mifugo na uvuvi yanatumika kuboresha hali ya lishe nchini.


Mkutano wa Usambazaji wa Nakala za Mpangokazi wa Utekelezaji wa Programu ya Unywaji Maziwa Shuleni ulienda sambamba na makabidhiano ya Vibanda vitakavyotoa huduma ya maziwa shuleni yalifanyika na Naibu Katibu Mkuu Mifugo Prof. Daniel Mushi katika Mji wa Serikali Mtumba.