Press Release
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MEI 24, 2024
MAADHIMISHO YA KITAIFA YA WIKI YA MAZIWA 2024 – MWANZA
Ndugu Wanahabari,
Bodi ya Maziwa Tanzania, Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuboresha unywaji wa maziwa na bidhaa zake na kuboresha soko la maziwa kila mwaka imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Maziwa Kitaifa ambayo huwa inafanyika kuanzia mwishoni mwa mwezi Mei hadi mwanzoni mwa mwezi Juni. Mwaka huu wa 2024 Wiki hii kitaifa itafanyika Mkoani MWANZA kuanzia Tarehe 28 Mei hadi Juni 1, 2024 katika Viwanja vya FURAHISHA Jijini Mwanza.
Tangu 1998 hii imekuwa shughuli ya kila mwaka na kwa mwaka huu ni Maadhimisho ya 27. Mwaka uliopita yaani 2023 yamefanyika Mkoani Tabora na sasa Mwaka 2024 Maadhimisho haya yatafanyika Mkoani MWANZA.
Ndugu Wanahabari,
Malengo ya Wiki ya Maziwa ni kama yafuatavyo:
- Kuelimisha wananchi na umma matumizi ya maziwa kama chakula bora kwa watu wa rika zote na faida za maziwa katika kujenga afya ya binadamu.
- Kuwashawishi watunga sera umuhimu wa tasnia ya maziwa katika kukuza uchumi wa nchi na kuondoa umasikini. Kutokana na kufuga ng’ombe wa Maziwa mfugaji anawezeshwa:
- Kumiliki mali yenye thamani kubwa kwani ng’ombe mmoja wa maziwa huwa na thamani ya zaidi ya shilingi za kitanzania milioni mbili (Tshs. 2,000,000.00)
- Kuondoa umaskini wa kipato kwa kupata fedha kutokana na mauzo ya maziwa yanayofanyika kila siku ambayo kwa mwaka mzima huweza kufikia shilingi za kitanzania million moja (Tshs. 1,000,000.00) kwani ng’ombe wa maziwa huweza kutoa maziwa hadi lita kumi kwa siku na hivyo kuwa na ziada ya kuuza baada ya kutoa matumizi ya nyumbani
- Kuongeza kipato kwa kuuza mitamba wa ziada na madume kwani kwenye ufugaji wa ng’ombe wa maziwa mfugaji hahitaji kuwa na kundi kubwa la ng’ombe
- Kupata maksai wakubwa na wenye nguvu zaidi na samadi kwa ajili ya kilimo cha mazao mengine
- Kuongeza ajira kwani kwa kila lita 100 za maziwa zinazouzwa kwa mwaka huzalisha nafasi nne (4) za ajira ya kudumu.
- Kuwaelimisha wadau kuongeza ubora wa bidhaa za maziwa zinazotengenezwa nchini
- Kujifunza teknolojia mpya za malisho, ukamuaji na usindikaji.
- Kuwaelimisha Wadau umuhimu wa kujiunga na vyama vya Ushirika
- Kuwa na jukwaa linalowakutanisha wadau wa tasnia ya maziwa ambao litawawezesha kubadilishana ujuzi na uzoefu na kujifunza baina ya wadau wa maziwa. Kwahiyo, katika Wiki ya Maziwa shughuli zingine muhimu za wadau zinafanyika sambamba na maonesho nazo ni Mkutano wa Baraza la Wadau wa Maziwa ambalo lipo Kisheria, Jukwaa la Wadau wa Maendeleo la Tasnia ya Maziwa
- Kuwahamasisha wadau kunywa maziwa yaliyosindikwa kwa ajili ya usalama na ubora wake
Ndugu Wanahabari,
Katika kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kitaifa matukio mengine yanakuwa yanaendelea ambayo ni kama ifuatavyo;-
28.05.2024 Kuanza kwa Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa na kugawa maziwa kwa makundi ya watu wenye mahitaji Maalumu.
29.05.2024 Uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa.
30.05.2024 Kongamano la Wadau.
31.05.2024 Ziara za Mafunzo.
01.06.2024 Kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maziwa 2024.
Ndugu Wanahabari,
Maadhimisho haya yanahusisha wadau mbalimbali katika Tasnia ya Maziwa, kuanzia uzalishaji, usindikaji na watumiaji wa maziwa na bidhaa zake. Mwaka huu katika kuadhimisha Wiki ya Maziwa tunashirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo kupitia mradi shirikishi wa wasindikaji na wazalishaji wa maziwa (TI3P) ambao wana mchango mkubwa katika kuwawezesha wafugaji mikopo ya Ng’ombe bora wa maziwa na mikopo ya uwekezaji katika viwanda vya kusindika maziwa.
Ndugu Wanahabari,
Kila mwaka maadhimisho huwa na kaulimbiu ya kitaifa ambayo hulenga kutoa ujumbe maalum kwa watanzania kwa mwaka husika. Hivyo basi maadhimisho haya mkoani Mwanza yatakuwa na dhana ya kuongeza ufanisi katika uzalishaji maziwa na kuyaongezea thamani Maziwa yaani kuyasindika ili kuhakikisha wananchi wanatumia Maziwa yaliyo salama kwa Afya zao. Wiki ya Maziwa iwe fursa ya kuhamasisha wadau na viongozi wa Mkoa wa Mwanza kuongeza tija katika uzalishaji na usindikaji wa maziwa na hitimaye kupunguza umasikini na kuongeza lishe kupitia matumizi ya Maziwa salama yaliyosindikwa. Ili kufikisha ujumbe huu muhimu wa Wiki ya Maziwa katika kuboresha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na usindikaji, uchumi wa viwanda, lishe na afya ya binadamu kauli mbiu ya mwaka 2024 Mkoani Mwanza inasema:
‘‘KUNYWA MAZIWA SALAMA KWA AFYA BORA NA UCHUMI ENDELEVU”
Mwisho
Bodi ya Maziwa Tanzania, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tunaendelea kutoa wito kwa Wadau wote wa Tasnia ya Maziwa na wananchi wote kwa ujumla kutumia fursa hii kushiriki katika Maadhimisho haya kuanzia Tarehe 28 Mei hadi Juni 1, 2024 katika Viwanja vya FURAHISHA katika Jiji la Mwanza.
Asanteni kwa kunisikiliza.