TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI SIKU YA UNYWAJI MAZIWA SHULENI GEITA  
                            
                            
                                          
                        
   
                    TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAADHIMISHO YA KITAIFA YA SIKU YA UNYWAJI MAZIWA SHULENI 2025 – GEITA
Ndugu Wanahabari,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bodi ya Maziwa Tanzania kwa kushirikiana na Mkoa wa Geita tunayo furaha kuwatangazia wadau wote wa Tasnia ya Maziwa na Umma kwa ujumla kuwa tutaadhimisha Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni kwa Mwaka 2025 Kitaifa Tarehe 24 Septemba 2025 mkoani GEITA.
Programu ya Unywaji Maziwa shuleni ilianzishwa mwaka 2000 na wadau wa mpango wa maziwa shuleni duniani kwa uratibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO). Wadau waliona kuwa kuna umuhimu wa kuwa na Siku maalumu ya kuadhimisha programu ya Unywaji wa Maziwa Shuleni. Wadau hao walikubaliana kuwa Jumatano ya mwisho wa mwezi Septemba kila mwaka iwe ndiyo Siku ya Maziwa Shuleni Duniani. Hii ni kutokana na kuwa Siku hiyo shule zote za msingi duniani huwa ni siku ya masomo.
Kwa Tanzania mwaka 2007 siku hiyo iliadhimishwa kitaifa kwa mara ya kwanza mkoani Kilimanjaro. Tangu hapo maadhimisho yamekua yakifanyika kila mwaka hapa nchini. Mwaka 2025 maadhimisho hayo yatafanyika mkoani wa GEITA.
Ndugu Wanahabari,
Kama tunavyofahamu watoto wengi nchini huenda shuleni asubuhi bila kula chakula chochote. Hii ina maana kuwa watoto hawa tangu walipokula chakula jana yake hawatapata chakula tena mpaka watakaporudi nyumbani saa nane hadi saa tisa mchana. Kwa watoto hiki ni kipindi kirefu sana kukaa bila chakula. Kwa hiyo watoto hawa huwa na njaa tangu wanapoanza masomo. Hali hii husababisha watoto hawa kuchoka haraka na kuanza kusinzia wakiwa darasani na hivyo kukosa mafunzo wanayopewa na walimu wao. Kutokana na hali hii, imeonekana kuwa mtoto akipata chakula kidogo katikati ya siku huwa mchangamfu na kufuatilia masomo vizuri.
Wataalamu wa lishe wanashauri kuwa chakula anachopewa mtoto kiwe na viinilishe vyote vinavyotakiwa kwenye chakula bora, yaani kiwe na wanga, protini, mafuta, vitamini, madini na maji ya kutosha. Ili kupata chakula cha namna hii ni lazima kuchanganya vyakula vya aina nyingi na kuhitaji maandalizi marefu. Mchanganyiko huu wa viini lishe vinapatikana kwa pamoja katika uwiano mzuri katika maziwa na maziwa yaliyosindikwa hayahitaji maandalizi ya ziada. Kwa hiyo wataalamu wa lishe wanashauri kuwa mtoto akipata glasi moja ya maziwa katikati ya siku amepata lishe ya kumtosha hadi atakaporudi nyumbani.
Ndugu Wanahabari,
Madhumuni makubwa ya maadhimisho haya ni kuwa na siku moja ambayo fikra za watu wote zitaelekezwa kwenye manufaa ya mpango wa maziwa shuleni na hivyo kuhamasisha kuanzishwa kwa mpango huu. Umuhimu wa siku hii ni kuwakumbusha wazazi umuhimu wa lishe bora kwa watoto hususani matumizi ya maziwa kwa maendeleo ya ukuaji wa mtoto. Watoto wawapo shule watumie maziwa
Umuhimu wa siku hii unatokana na kuwa nchi nyingi zinafanya kitu kile kile siku hiyo hiyo na kuungwa mkono na Shirika la Chakula Duniani (FAO) na hivyo kuonyesha kuwa program hizi zinawezekana. Aidha maadhimisho haya yanawatia shime wale ambao tayari wameanza na kuwashawishi wale ambao hawajaanza waanzishe mpango huu kwa watoto wao.
Ndugu Wanahabari,
Kwenye nchi ambapo wanaendesha mpango wa maziwa shuleni wameorodhesha manufaa yafuatayo kwa watoto:
• Kuboresha ukuaji wa watoto
• Watoto wanakuwa na afya bora
• Kupata matokeo mazuri zaidi kitaaluma
• Kuanza mapema kuwa na tabia ya lishe bora ambayo ni sehemu ya kuboresha/kuimarisha afya
• Mahudhurio mazuri shuleni, utoro kupungua na kupungua idadi ya watoto wanaoacha shule
• Kuwa na raia wenye afya bora baada ya watoto hawa kumaliza shule.
• Kupanua utamaduni wa kunywa maziwa kwenye jamii na hivyo kuongeza wastani wa kunywa maziwa kwa kila mtu nchini.
• Kuchangia pato ghafi la taifa
Ndugu Wanahabari,
Katika kuelekea Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni matukio mengine yanakuwa yanaendelea ambayo ni kama ifuatavyo;
• Kugawa Maziwa kwa watoto wa shule zenye mahitaji maalumu tarehe 22.09.2025
• Kikao cha Kongamano la Wadau wa Maziwa Nchini litakalofanyika Tarehe 23.09.2024, kwenye Ukumbi ulipo Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ndugu Wanahabari,
Kila mwaka Maadhimisho haya huwa na kaulimbiu ya Kitaifa ambayo hulenga kutoa ujumbe maalumu kwa watanzania kwa mwaka husika. Hivyo basi kwa mwaka huu Maadhimisho haya Mkoani GEITA yatakuwa na kaulimbiu isemayo
‘’KWA MATOKEO MAZURI SHULENI NA AFYA BORA, MAZIWA NDIO MPANGO MZIMA”
Kaulimbiu hii ina dhana ya kutoa hamasa kwa wazazi na walimu kuhakikisha unywaji wa maziwa kwa wanafunzi ni endelevu kwa kuzingatia umuhimu wa maziwa katika kuimarisha afya ya mwili na ukuaji wao kwa ujumla ambapo kwa pamoja husaidia sana kwenye kufaulu masomo yao.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Bodi ya Maziwa Tanzania tunaendelea kutoa wito kwa wazazi, walimu na wanafunzi kutumia maziwa wawapo shuleni na nyumbani. Aidha, niwakaribishe wananchi wote, wazazi, wanafunzi, wadau wote wa Tasnia ya Maziwa kushiriki katika Maadhimisho haya siku ya Tarehe 24 Septemba, 2025 katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo Manispaa ya Geita.
Ni matumaini yangu kuwa maadhimisho haya ya Siku ya unywaji Maziwa Shuleni yatakuwa fursa kubwa kwenu wazazi na walimu katika kuhakikisha mnaboresha afya za wanafunzi.
Karibuni sana.
Asanteni kwa kunisikiliza.
 
            