HOTUBA WIKI YA MAZIWA MRORGORO 2025
HOTUBA YA MGENI RASMI MKUU WA MKOA WA MOROGORO MHESHIMIWA ADAM KIGHOMA MALIMA SIKU YA UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA 28 YA WIKI YA MAZIWA NA UZINDUZI WA KAMPEINI YA KUHAMASISHA UNYWAJI WA MAZIWA NCHINI KATIKA UWANJA WA ZIMA MOTO(FIRE) MKOA WA MOROGORO
TAREHE 28 MEI, 2025
Katibu Mkuu Wizara Mifugo na Uvuvi,
Katibu Tawala wa Mkoa Morogoro,
Msajili wa Bodi ya Maziwa
Wakuu wa Wilaya,
Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro,
Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya,
Wakurugenzi wa Halmashauri mbalimbali,
Wawakilishi wa Sekta Binafsi,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Ndugu wananchi; Awali ya yote, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kutufikisha siku ya leo salama. Pia nichukue nafasi hii kumkaribisha kila mmoja katika Mkoa wa Morogoro na kushiriki maadhimisho ya wiki ya Maziwa yanayofanyika kitaifa katika Mkoa wetu wa Morogoro.
Ndugu Wananchi; Kama mnavyofahamu kuwa Nchi yetu imekuwa ikiadhimisha Wiki ya maziwa kila Mwaka kuanzia Mwaka 1998. Maadhimisho haya huanzia tarehe 28 Mei hadi 01 Juni kila Mwaka ambapo tarehe 01 Juni huwa ni siku rasmi na mahususi ya kilele cha Wiki ya Maziwa.
Ndugu Wananchi; Mwaka huu Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa nafasi kwa Mkoa wa Morogoro kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya kitaifa. Hii ni kutokana na Mkoa huu kuwa miongoni mwa Mikoa ya Tanzania yenye Ng’ombe wengi takribani 2,039,056 ambapo Ng’ombe wa asili ni 1,965,847 na Ng’ombe wa maziwa walioboreshwa ni 73,209.
Ndugu Wananchi; Kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa Mwaka huu ni “Maziwa Salama kwa Afya Bora na Uchumi Endelevu”. Kauli mbiu hii inalenga na kusisitiza umuhimu wa maziwa katika kupunguza umaskini kwa kuongeza kipato na ajira katika kaya, kuboresha lishe na afya ya jamii. Kwa maana hiyo mtu akiwa na afya bora na kipato cha uhakika itamfanya afurahie maisha pamoja na familia yake na hivyo kujiletea maendeleo yeye na Taifa kwa ujumla.
Ndugu Wananchi; Kufanyika kwa maadhimisho ya Wiki ya unywaji wa maziwa katika Mkoa wetu inalenga pia kutoa hamasa kwa jamii kujiwekea utaratibu wa kunywa maziwa kiasi cha lita 200 za maziwa kwa Mwaka kwa mujibu wa viwango vinavyopendekezwa na Shirika la Chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Kiwango cha unywaji wa maziwa katika Nchi yetu kwa sasa kiko chini sawa na wastani wa lita 68.1 kwa mtu kwa Mwaka.
Ndugu Wananchi; Kutokana na ratiba, maadhimisho haya yatafanyika kuanzia leo Jumatano tarehe 28 Mei, 2025 hadi tarehe 01 Juni, 2025 ambayo ni siku ya kilele cha Wiki ya Maziwa Kitaifa. Hivyo nitumie nafasi hii kuwaasa Wananchi wa Mkoa wa Morogoro, Wadau wa maziwa na Sekta binafsi kuitumia fursa hii ya maadhimisho haya kuhudhuria na kujifunza namna ya ufugaji bora wa Ng’ombe, ili kuongeza uzalishaji wa maziwa, Upimaji ubora na usindikaji wa maziwa. Ni matumaini yangu kuwa maadhimisho haya ya wiki ya maziwa yatakuwa fursa kubwa kwenu katika kuwahamasisha kuongeza uzalishaji wa maziwa na hivyo kusaidia kuongeza kipato na lishe bora.
Ndugu Wananchi; Baada ya kusema hayo napenda kuchukua nafasi hii kutamka rasmi kwamba maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kitaifa kwa Mwaka huu 2025 yamefunguliwa Rasmi.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
