Virutubisho gani vinapatikana kwenye maziwa?
Virutubisho vinavyopatikana kwenye maziwa Maziwa hutupatia takriban vitamini zote ambazo huyeyuka kwenye mafuta. Nazo ni vitamini A, D, E na K. Vitamini A huhusika na shughuli mbalimbali mwilini. Mfano afya bora ya ngozi zetu kuwa nyororo na ng'avu na pia kuwa na uwezo wa kuzuia wadudu wasiingie mwilini. Vile vile vitamini A hutumika pia kuyapatia macho uimara wa kuona. Na hasa kuona usiku au kwenye mwanga hafifu. Ukosefu wake hudhoofisha macho na hata kuleta upofu, ngozi kusinyaa na kuonekana iliyozeeka hata kama ni ya kijana. Vitamini D husaidia mwili kuweza kufyonza madini ya kalsiamu. Bila kuwepo vitamni D kalsium hupotea bure kwa kutolewa nje kama kitu kichohitajika. Japokuwa vitamini D tunaweza kuipata kwenye jua la asubuhi, watu wengi hawawezi kulipata jua hilo. Labda kwa kuishi magorofani au chini ya milima au kutoweza kutoka nje nyakati za asubuhi. Hivyo ni bora kujiwekea uhakika wa kupata vitamini D kwa kunywa maziwa. Umuhimu wa madini ya Calcium ni kiungo muhimu katika ujengaji wa mifupa. Hasa kwa wajawazito na watoto ambao mifupa yao bado inajengeka. Mwili imara hubebwa na mifupa imara. Na mifupa imara inajengwa na madini ya Kalsium. Ni bora kujijengea mifupa imara, meno na sehemu ya mifupa. Hakika kila mtu anahitaji meno bora na imara, vile vile kalsium hutumika katika misuli (muscle) wakati wa kujikunja na kunyooka. Pia husaidia katika mtandao wa ufahamu mwilini (nerve conduction). Kwa ufupi hayo ni manufaa ya kunywa maziwa, samaki na kadhalika. Mbali na Kalsium maziwa hutupatia madini ya salfa, sodium na phosphoras ambayo mwili pia huhitaji kwa kazi zake mbalimbali. Maziwa pia hutupatia protini kwa ujengaji wa miili yetu. Mathalan mtoto mdogo wa siku moja huongeza ukubwa na uzito kwa kunywa au kunyonya maziwa tu. Japokuwa kiwango cha protini hutofautiana kulingana na mnyama, pia maziwa ya ng'ombe yana protini ya kutosha. Hali kadhalika katika maziwa ya mbuzi na kadhalika. Maziwa pia hutupatia sukari (wanga) japo kwa kiasi kidogo lakini kidogo chafaa kuliko kukosa. Na ndio maana japo kwa kunywa maziwa waweza kuhisi nguvu iwapo ulikuwa na njaa. Nyakati za baridi, maziwa hutumika kama kinywaji moto. Yenyewe peke yake kwenye chai, kahawa au tangawizi. Na wakati wa joto, maziwa hutumika kama kipozeo na kiburudisho tosha. Na kwa nyakati hizi, kila sehemu inaweza kupatikana na maziwa. Kwa asiyependa tunamshauri aanze kuyapenda na kuyatumia. Maziwa pia hutumika kama dawa kwa kuchanganywa na vitu mbalimbali. Mathalani maziwa ya mama yakamuliwapo kwenye jicho linalowasha, uchafu hotoka na kujihisi salama. Kwa kuzingatia umuhimu wa maziwa kama tulivyoona kwa ufupi, kwa kauli moja tunaisisitiza jamii kunywa maziwa katika milo ya kila siku. Na vile vile kama kiburudisho wakati wowote. Ni hasara kupoteza fedha zako kununua vinywaji visivyo na faida kubwa kama tuipatavyo katika maziwa, mathalan soda, na juice za makopo ambazo zimejaa rangi, maji na sukari na madawa bila ya virutubisho vyovyote vingine. Tumia pesa zako kwa malengo maalum. Jenga afya yako, kunywa maziwa.