11 Wasajiliwa Maonesho ya Sabasaba 2025

Wadau wa maziwa wapatao 11 wamesajiliwa na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) kwenye mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Mifugo (mimis) wakati wa maonesho ya 49 ya Kimataifa yakibiashara yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam ikiwa ni moja ya shughuli zilizofanyika na TDB wakati wa maonesho hayo.
Usajili huo wa wadau wanaojihusisha katika mnyororo wa thamani wa maziwa unamuwezesha mdau wa maziwa kutambulika na bodi ambayo ndio imepewa dhamana ya kisheria kusimamia Tasnia ya Maziwa vilevile humuwezesha mdau kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo mbalimbali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau hao wameishukuru Bodi ya Maziwa Tanzania kwa miongozo mbalimbali walioipata kabla hawajasajiliwa kwakuwa wengi hawakuwa na ufahamu wa sheria ya maziwa na miongozo yake hali iliyopelekea kufanyabiashara ya maziwa bila kuwa na kibali kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania.
Awali akiongea na wadau hao kwa nyakati tofauti Mtekinolojia wa Chakula Mwandamizi kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania Bw. Dotto Nkuba amewataka wadau wote wa maziwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazotakiwa kufuatwa kwenye Tasnia ya maziwa kwa maendeleo ya Tasnia ya Maziwa hapa nchini.