BODI YA MAZIWA YASISITIZA UNYWAJI WA MAZIWA KUBORESHA AFYA NA UKUAJI WA WATOTO
Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) imesisitiza umuhimu wa kuhamasisha unywaji wa maziwa kwa watoto ili kuboresha afya, ukuaji na lishe bora, hususan katika kipindi cha ukuaji. Wito huo umetolewa na Meneja Masoko wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Bw. Joseph Semu, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga.
Bw. Semu amesema maziwa ni miongoni mwa vyakula vyenye virutubisho muhimu vinavyochangia ukuaji wa mifupa na meno, kujenga na kurekebisha tishu za mwili pamoja na kusaidia ukuaji wa watoto. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wanapata lishe yenye mchanganyiko wa vyakula mbalimbali, ikiwemo maziwa, kulingana na mahitaji yao ya lishe.
Aidha, ameeleza kuwa kuimarisha unywaji wa maziwa kwa watoto kunahitaji ushirikiano wa wazazi, shule, Serikali na wadau wa tasnia ya maziwa ili kuongeza uelewa kuhusu manufaa ya maziwa na kuweka mazingira yanayorahisisha upatikanaji wake. Ameongeza kuwa elimu kuhusu ubora na usalama wa maziwa ni muhimu ili kuhakikisha wananchi wanatumia maziwa salama na yenye ubora unaotakiwa.
Akizungumzia ushiriki wa Bodi katika Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, Bw. Semu amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kuelimisha jamii kuhusu mchango wa maziwa katika lishe bora na kuhamasisha uzalishaji pamoja na matumizi yake nchini. Kupitia elimu hiyo, TDB inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu thamani ya maziwa katika afya na maendeleo ya watoto na jamii kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa juhudi za kuongeza matumizi ya maziwa zinapaswa kwenda sambamba na kuimarisha uzalishaji, ubora na usalama wa maziwa ili wananchi waweze kuyapata kwa urahisi na kwa gharama zinazomudu. Hatua hiyo ni muhimu katika kujenga jamii yenye uelewa wa lishe bora na kuchochea maendeleo ya tasnia ya maziwa nchini.
