NAIBU WAZIRI SILINDE ATEMBELEA BANDA LA TDB MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI TANGA
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, Leo Oktoba 12, 2026 ametembelea Banda la Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) katika Ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uzalishaji wa chakula na kuhakikisha wananchi wanapata lishe bora kwa maendeleo ya afya na ustawi wao.
Akiwa katika banda hilo, Mhe. Silinde amepata maelezo kuhusu majukumu na shughuli zinazotekelezwa na Bodi ya Maziwa Tanzania katika kuendeleza Tasnia ya Maziwa nchini, hususani katika kuhamasisha uzalishaji, usalama na ubora wa maziwa pamoja na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa maziwa katika lishe bora.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa Tasnia ya Maziwa ili kuongeza uzalishaji na matumizi ya maziwa nchini, hatua itakayochangia kuboresha lishe ya wananchi na kukuza uchumi kupitia shughuli za ufugaji na biashara ya maziwa.
Akizungumza katika banda hilo, Meneja Masoko wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Bw. Joseph Semu, amesema kuwa Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa inayotekeleza Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP), unaolenga kuimarisha Tasnia ya Maziwa na kuongeza uwezo wa wadau kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Bw. Semu ameeleza kuwa kupitia mradi huo, juhudi zinaelekezwa katika kuimarisha uzalishaji endelevu wa maziwa, kuboresha mifumo ya ufugaji na kuendeleza biashara ya maziwa, sambamba na kuhamasisha matumizi ya maziwa kwa ajili ya lishe bora.
Ushiriki wa TDB katika maadhimisho hayo ni sehemu ya juhudi za kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa maziwa na mchango wake katika kuboresha lishe na kukuza uchumi wa wananchi.
