KURARAY YA JAPAN KUONESHA NIA YA KUWEKEZA KWENYE VIFUNGASHIO VYA MAZIWA TANZANIA
Kampuni ya Kuraray kutoka nchini Japan, inayojishughulisha na teknolojia na uzalishaji wa vifungashio kwa ajili ya bidhaa za maziwa, imeonesha nia ya kuwekeza katika eneo la vifungashio ndani ya Tasnia ya Maziwa nchini Tanzania.
Nia hiyo ilielezwa Novemba 25, 2026, wakati ujumbe wa kampuni hiyo ulipotembelea Ofisi za Makao Makuu ya Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), jijini Dodoma, na kufanya mazungumzo na Msajili wa Bodi hiyo, Prof. George Msalya.

Akizungumza katika mazungumzo hayo, Prof. Msalya aliwakaribisha wawakilishi wa Kuraray na kueleza kuwa uwekezaji katika teknolojia za vifungashio ni muhimu katika kuongeza ubora, usalama na muda wa matumizi ya bidhaa za maziwa, pamoja na kuimarisha ushindani wa bidhaa hizo katika soko.
Kwa upande wake, Bi. Maya Murakami, Mtaalamu wa Maendeleo ya Masoko kutoka Kuraray, alieleza nia ya kampuni hiyo kushirikiana na wadau wa Tanzania katika kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa za vifungashio zitakazosaidia kuongeza thamani ya bidhaa za maziwa na kukuza fursa za biashara katika tasnia hiyo.
Naye Bw. Yusushi Morihara, Meneja wa Huduma za Kitaalamu na Maendeleo ya Masoko wa kampuni hiyo, alieleza umuhimu wa kutumia teknolojia sahihi za vifungashio katika kuhakikisha bidhaa za maziwa zinahifadhi ubora na usalama wake katika hatua mbalimbali za uzalishaji, uhifadhi na usambazaji.

Katika hatua nyingine, Prof. Msalya aliitaja Kampuni ya Kuraray kuwa mdau muhimu anayeweza kuchangia juhudi za kuimarisha matumizi ya maziwa nchini, huku akiiomba kampuni hiyo kuunga mkono Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni unaolenga kuongeza matumizi ya maziwa miongoni mwa watoto na kuboresha lishe zao.
Ombi hilo lilikubaliwa na wawakilishi wa kampuni hiyo, hatua inayofungua fursa ya ushirikiano kati ya Kuraray na Bodi ya Maziwa Tanzania katika kuendeleza matumizi ya maziwa na kukuza Tasnia ya Maziwa nchini.
