Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
WANGING’OMBE YATAKA MPANGO WA MAZIWA SHULENI KUCHOCHEA UFUGAJI WA NG’OMBE WA MAZIWA
13 Nov, 2026
WANGING’OMBE YATAKA MPANGO WA MAZIWA SHULENI KUCHOCHEA UFUGAJI WA NG’OMBE WA MAZIWA

Wananchi wa Kata ya Wanging’ombe wametakiwa kutumia fursa ya Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni kukuza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya shule na kukuza kipato cha kaya.

Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata ya Wanging’ombe, Bw. Geoffrey Nyagawa, wakati akifungua kikao kilichowakutanisha Kamati ya Shule, wawakilishi wa wazazi na viongozi wa Serikali ya Kijiji pamoja na wataalamu kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe na Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe.

Bw. Nyagawa alisema mpango huo ni fursa muhimu kwa wananchi kujikita katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ili kuongeza upatikanaji wa maziwa kwa ajili ya wanafunzi. Aidha, alihimiza shule za jirani kuanzisha mpango huo ili manufaa yake yawafikie wanafunzi wengi zaidi.

Akizungumza katika kikao hicho, Meneja Masoko wa TDB, Bw. Joseph Semu, alieleza umuhimu wa ushiriki wa wazazi, viongozi wa jamii na wadau wengine katika kuweka mikakati ya kuanzisha na kuendeleza Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni kwa manufaa ya wanafunzi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP) katika Halmashauri ya Wanging’ombe, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Winson Mfikwa, alisema mradi huo una nafasi muhimu katika kuendeleza Tasnia ya Maziwa wilayani humo kwa kusaidia kuboresha uzalishaji, kuongeza tija kwa wafugaji na kujenga uwezo wa wadau katika mnyororo wa thamani wa maziwa. Alieleza kuwa kupitia ushirikiano na wadau, mradi unalenga kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa maziwa na kukuza fursa za kiuchumi zinazotokana na shughuli za uzalishaji na biashara ya maziwa.

Naye Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wanging’ombe, Bw. John Deus, alieleza kuwa maziwa ni chakula chenye virutubisho muhimu vinavyosaidia ukuaji na maendeleo ya mtoto. Alisisitiza kuwa ulaji wa maziwa kama sehemu ya lishe bora unaweza kuchangia ukuaji wa ubongo na uwezo wa mtoto kujifunza, hivyo akawahimiza wazazi kushiriki katika kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe yenye ubora.

Akizungumzia ushiriki wa kampuni yake katika mpango huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kend’s Milk, Bw. God Nungwi, alisema kampuni hiyo itashirikiana na shule na wadau kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma bora za maziwa kwa kuzingatia mahitaji yao. Alieleza kuwa kampuni itazingatia upatikanaji wa maziwa yenye ubora na usalama, pamoja na utaratibu wa kuyafikisha shuleni kwa wakati, kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika kikao hicho.

Kupitia C-SDTP, TDB inaendelea kushirikiana na Serikali za Mitaa, shule, wazazi na wadau wa Tasnia ya Maziwa kuhamasisha uanzishwaji wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni, unaolenga kuboresha lishe ya wanafunzi na wakati huohuo kukuza uzalishaji na soko la maziwa kwa manufaa ya wafugaji na wadau wengine.