Prof. Msalya: Maziwa kwa Wanafunzi, Chachu ya Ufaulu Shuleni

Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Prof. George Msalya amesema kuwa matumizi ya maziwa kwa wanafunzi ndio chachu ya ufaulu mzuri wawapo shuleni sambamba na kuimarisha afya ya mwili na ukuaji wao kwa ujumla ambapo kwa pamoja husaidia sana kwenye kufaulu masomo yao
Ameyasema hayo leo Septemba 18, 2025 alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya Bodi ya Maziwa Tanzania jijini Dodoma akiwa anaelezea Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni yanayotarajiwa kufanyika Septemba 24, 2025 Mkoani Geita ambapo ametoa wito kwa wazazi, walimu na wanafunzi kutumia maziwa wawapo shuleni na nyumbani ili kuimarisha afya ya mwili.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote, wazazi, wanafunzi na wadau wote wa Tasnia ya Maziwa nchini kushiriki katika maadhimisho hayo siku ya tarehe 24 Septemba, 2025 yatakayofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo Manispaa ya Geita.
‘Ni matumaini yangu kuwa maadhimisho haya ya Siku ya unywaji Maziwa Shuleni yatakuwa fursa kubwa kwenu wazazi na walimu katika kuhakikisha mnaboresha afya za wanafunzi.’ Amesisitiza Prof. Msalya
Msalya ameongezea kuwa katika kuadhimisha siku hii huambatana na matukio mengine kama vile kugawa maziwa kwa wanafunzi kwenye shule zenye mahitaji maalumu pamoja na Mkutano wa wadau wa maziwa walioko Geita ili kuwaunganisha pamoja kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika Tasnia ya Maziwa.
Kwa mwaka huu Maadhimisho haya yatabebwa na kauli mbiu isemayo “Kwa Matokeo Mazuri Shuleni na Afya Bora, Maziwa ndio Mpango Mzima” ambapo ina dhana ya kutoa hamasa kwa wazazi na wali,u kuhakikisha unywaji wa maziwa kwa wanafunzi ni endelevu kwa kuzingatia umuhimu wa maziwa katika kuimarisha afya ya mwili na ukuaji wao kwa ujumla.