Imewekwa: 29th Nov, 2022
Chama cha Ushirika cha Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) kimeshauri kuwa uthibiti ubora wa maziwa uanzie kwa wafugaji kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wafugaji hao ikiwa ni pamoja na kukagua vyombo vinavyotumika kuhifadhia maziwa hayo pamoja na kuwafundisha namna ya kukamua maziwa ili kuhakikisha hawabakizi maziwa kwenye kiwele cha ng’ombe.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa Chama hicho Ndg. Shamte Said kwenye ziara ya Bodi ya Ushauri ya Bodi ya maziwa Tanzania walipowatembelea Novemba 24, 2022 kutaka kujua maendeleo ya chama hicho kwa ujumla na changamoto zinazokikabili chama hicho kwa sasa.
Akieleza hali ya chama hicho mbele ya bodi hiyo, mwenyekiti wa TDCU amesema kuwa kwa sasa chama kinapitia changamoto kadhaa kama vile uhaba wa maziwa yanayotakiwa kupelekwa kiwandani kwa ajili ya kuchakatwa hali iliyosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi kiasi kwamba kiangazi kimekuwa cha muda mrefu ukilinganisha na kipindi cha mvua ambapo kwa sasa maziwa yanayopatikana kwa ajili ya uchakataji ni lita 10,000 tu kwa siku ikilinganishwa na lita 40,000 kwa siku kipindi cha mvua.
Vilevile mwenyekiti huyo alibainisha kuwepo kwa vituo vya kukusanyia maziwa vilivyo nje ya mfumo rasmi ni changamoto nyingine inayopitia chama hicho kwani hali hiyo ndio inayopelekea kukosekana kwa maziwa yakutosha kupeleka kiwandani kwa ajili ya uzalishaji hivyo ameitaka Bodi ya maziwa Tanzania kujipanga kuona namna ya kuthibiti vituo hivyo visivyo rasmi pamoja na maziwa yanayouzwa kiholela huko mtaani.
Changamoto nyingine alizozibainisha ni pamoja na bei ya maziwa kuwa chini kwa kipindi kirefu ukilinganisha na gharama za ufugaji kwa sasa hivyo hupelekea wanachama wengi kuuza maziwa yao kwa mfumo usio rasmi kwa bei iliyopo sokoni kwa sasa ili waweze kujikwamua na kukidhi gharama za ufugaji.
Hata hivyo pamoja na changamoto hizo wanazozipitia Chama kimejipanga kwa kujiwekea mikakati ya muda mfupi na mrefu ilikukabiliana nayo kama vile kuwa mkakati wa miaka 5 wa kuongeza uzalishaji na ukusanyaji wa maziwa, kuwatafutia wanachama mitamba bora, kuongeza sehemu za malisho pamoja na kuja na mpango mkakati wa kuwashirikisha vijana kwenye tasnia ya maziwa mkoani Tanga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Maziwa Tanzania Profesa Zackaria Masanyiwa amekitaka chama hicho kuweka mikakati inayotekelezeka ilikukifanya chama kiweze kupiga hatua mbele zaidi, pia amesisitiza kuwa kuwepo kwa ushindani katika sekta ya maziwa iwe ni fursa kwa chama kufanya vizuri zaidi kudhibiti ubora wa maziwa.
Chama cha Ushirika cha Maziwa Tanga (TDCU) kilianzishwa Machi 1993 ikiwa na lengo la kukusanya maziwa kutoka katika vyama vidogovidogo vya ushirika wa maziwa vya mkoani Tanga na kuyapeleka kiwandani kwa ajili ya usindikaji. Kwa sasa chama kina wanachama wasiopungua 6000 wanaoleta maziwa kiwandani.