Imewekwa: 05th Dec, 2022
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Abdallah Ulega amehimizi matumizi ya Maziwa yanayozalishwa na viwanda vyetu vya ndani ili kujenga tabia ya kupenda vya kwetu.
Mheshimiwa Ulega ameyasema hayo Leo Desemba 3, 2022 katika bonanza la Maziwa lilioandaliwa Kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) pamoja na Klabu ya wanamichezo wa mbio za polepole ijulikanayo Kama "Dar Jogging Club".
Mhe. Ulega amesisitiza kuwa Maziwa yanayosindikwa na viwanda vyetu hapa nchini Kwa sasa yanaweza kukaa Kwa muda mrefu hali ambayo yanaweza kushindana na bidhaa yoyote ya maziwa yanayotoka nje ya nchi ambapo hapo awali hawakuweza kushindana kibiashara katika soko la nje.
"Niwaambie ndugu zangu, Kwa sasa baadhi ya wadau wa Maziwa wamejipanga kukabiliana na soko la Maziwa duniani Kwa kuzalisha Maziwa yanayoweza kudumu Kwa muda mrefu bila kuharibika na Kama hiyo haitoshi ndugu yetu Asas amejipanga zaidi kuanzisha kiwanda Cha kusindika Maziwa ya unga" amesa Mhe. Ulega
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) Bi. Latifa Khamis amesema kuwa maonesho ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini yamekuwa na lengo la kuwahasisha watanzania kupenda kutumia zaidi bidhaa zinazotengenezwa na wawekezaji wa hapa nchini Maziwa ikiwa ni mojawapo ili kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.
Naye Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Dkt. George Msalya wamewataka vijana kuchangamkia fursa zilizopo kwenye tasnia ya maziwa hapa nchini kwani Kwa sasa biashara ya maziwa inakua kwa kasi ikizingatiwa kuwa maziwa ni chakula kinachojitosheleza katika mfumo wa ukuaji wa binadamu.
Wiki ya Maonesho ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini yaliyobeba ujumbe usemao "tununue vya kwetu" yametanguliwa na mbio za polepole (jogging) zilizoongozwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) Bi. Latifa Khamis pamoja na Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Dkt. George Msalya ambapo zaidi ya vikundi 8 vya wakimbiaji vilishiriki.